vilabu

STAND WAPATA NEEMA, EXIM YAMWAGA NOTI

BENKI ya Exim imesaini makubaliano ya kuifadhili timu ya soka ya Stand United FC ya Shinyanga.

Hii ni timu ya kwanza kupata ufadhili kutoka Benki ya Exim. Ufadhili huo wa mwaka mmoja utaisaidia timu hiyo kushiriki katika Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa 2014/2015.

“Makubaliano haya yanaikutanisha Benki ya Exim na mchezo mkubwa kuliko yote Tanzania,” alisema Mkuu wa Matawi ya Benki ya Exim Kanda ya Ziwa, Justus Mukurasi jana katika hafla iliyofanyika mjini Shinyanga.

Mukurasi alisema hakuna mchezo wenye watazamaji, wafuatiliaji na mashabiki wengi zaidi nchini kama mpira wa miguu.

“Timu ya Stand United ina nguvu kubwa ya kuunganisha mashabiki wa Kanda ya Ziwa. Hivyo ni jambo stahiki kwa Benki ya Exim kuisaidia timu hii ambayo mashabiki wake ni miongoni mwa wateja wa Benki ya Exim,” alisema.

Mukurasi aliongeza kuwa pande hizo mbili zilifanikiwa kuingia katika makubaliano ambayo yataiwezesha benki hiyo kuifadhili Stand United tangu Ligi Kuu Tanzania Bara ilipoanza Septemba 20, mwaka huu.

“Kwetu sisi udhamini tuliofanya sio tu wa nembo, bali ni ufadhili wa muda mrefu utakaozinufaisha pande zote mbili,” aliongeza meneja huyo. “Tunatumaini kuwa kila mmoja wetu ataweza kujifunza kutoka kwa mwenzake ili kupata matokeo mazuri kwa pamoja. Exim itasaidia kukuza na kuendeleza mchezo wa soka na hivyo kuiwezesha benki yetu kuwa karibu zaidi na wateja wake,” alisema Mukurasi.

Naye Mwenyekiti wa Stand United FC, Aman Vicent alisema timu yake inayo furaha kubwa kuingia katika makubaliano na Benki ya Exim.

“Tunadhamiria kuimarisha uhusiano huu ili kuhakikisha timu yetu inafanya vizuri katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu,” alisema Vicent.

“Kwa niaba ya Stand United FC, ningependa kuishukuru Benki ya Exim kwa jitihada zao za kusaidia wachezaji wetu na timu kwa ujumla. Tunafanya kazi kubwa kuhakikisha tunainua vipaji vya wachezaji wetu ili na wao waweze kufika mbali zaidi,” aliongeza mwenyekiti huyo.



CHANZO: HABARI LEO

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.