zanzibar

KONGAMANO LA KATIBA ZFA KUFANYIKA KESHO KUTWA

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhPUP_TY6rf0eh23-pATqE8IWcpcOuQx_ERnTOk1c0gn8tyGztdlxr1fd39IJJjoqdnYbpAn2aF-Lc9BniCd_ijsGpYsCF6qf1cuQv2t8quY4FrNtVQc6JMHlRpoJ2loos4k8UBu8nLdkc/s1600/Zanzibar-Football-Association2.jpg
KONGAMANO la wazi litakalozungumzia juu ya katiba ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) linatarajiwa kufanyika keshokutwa visiwani Zanzibar.

Kongamano hilo ambalo limeandaliwa na Taasisi ya kuendeleza na Kukuza Michezo Zanzibar (ZANEP) mbali na katiba litajadili mustakabali wa michezo yote Zanzibar, litaoneshwa moja kwa moja na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC).

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Ocean View, jana Rais wa Taasisi hiyo Farouk Kareem alisema kongamano hilo litaanza saa 3:00 hadi saa 6:00 usiku.

Aidha alisema pamoja na kuwa ZFA ipo katika mchakato wa kuiandaa katiba, lakini lazima wakubali kuwa katiba iliyopo imeshapitwa na wakati na ni lazima wakubali kuifanyia marekebisho ili kufuta kilio kikubwa kwa Wazanzibari kuona wanataka Katiba mpya kwa mustakabali wa soka lao.
Alisema kongamano hilo litawashirikisha wadau mbali mbali ambao hawamo ndani ya chama hicho ili kutoa maoni yao.

“Tunajua kuwa hivi sasa kumekuwepo na mchakato wa katiba ya ndani ya chama hicho ambao unaendelea na sisi kama wadau tumeona ipo haja ya kufanya mjadala huo kuwashirikisha na wadau ambao hawamo ndani ya chama ili kutoa maoni yao,” alisema Farouk.

Alisema kuwa wakiwa katika harakati za kuendeleza soka wameona bado kuna tatizo la katiba ya chama ZFA kwa hivyo katiba hiyo ni lazima wakubali imeshapitwa na wakati na inahitaji kufanyiwa marekebisho.

“Hiki ni kilio kikubwa cha Wazanzibari kuona kama wanakuwa na katiba mpya yenye mwelekeo mpya ambayo itakubalika katika medali ya michezo,” alisema.

Alisema katika kongamano hilo mwanasheria wa kujitegemea ambae ni miongoni mwa waliomo kwenye kamati hiyo, Abdalla Juma atatoa mada juu ya katiba gani wanayoitaka ya ZFA na baadae watatoa fursa katika ukumbi huo kuchangia.

“Lengo letu ni kutoa mwamko kwa wadau wetu wa Zanzibar juu ya katiba hiyo,” alisema.

About Unknown

0 comments:

Powered by Blogger.