vilabu

MAKATA KOCHA KAGERA SUGAR, KABANGE ATIMKA



UONGOZI wa Kagera Sugar umempa mkataba wa mwaka mmoja Mbwana Makata kuwa kocha wa timu hiyo msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Timu hiyo imetangaza pia kuachana na kocha msaidizi Mrage Kabange, ambaye mkataba wake umekwisha.

Makata ambaye ameisaidia Tanzania Prisons kubaki Ligi Kuu msimu huu, ameingia mkataba na Kagera Sugar hivi karibuni akichukua mikoba ya aliyekuwa Kocha Mkuu Jakson Manyanja.

Akizungumza na gazeti hili jana Katibu Mkuu wa Kagera Sugar, Hamis Madaki alisema wameamua kumpa Makata mkataba wakiamini atakisaidia kikosi cha Kagera Sugar kufanya vizuri zaidi msimu ujao.

Pia, alisema wamechana na Kabange na sasa wanatafuta Kocha Msaidizi mwingine ambaye atasaidiana na Makata kukiwezesha kikosi hicho kuchukua taji la ubingwa msimu ujao.

“Tumeachana na makocha wote, tunataka kupata changamoto mpya ambazo zitasaidia kikosi chetu kusonga mbele zaidi, ikiwezekana kuchukua taji msimu ujao,”alisema.

Kuhusu usajili Katibu huyo alisema wanampa Makata muda kidogo ili ajipange na kuwaeleza anahitaji wachezaji wa aina gani ambao watafanya vizuri na siku sio nyingi watatangaza usajili wao.

“Kocha wetu bado ni mpya ndio kwanza tumesaini naye mkataba hivyo ni mapema kuzungumza ni lini tutafanya usajili, lakini mipango ipo,”alisema.

Katika mahojiano na Kabange kuhusu kuachwa kuifundisha Kagera, alisema hajui na kwamba pengine uongozi huo unataka mabadiliko mapya lakini ukweli mkataba wake umekwisha.

“Unajua tena makocha tunaajiriwa kwa ajili ya kufukuzwa, sijui kwanini hawakunipa mkataba mwingine labda walitaka kufanya mabadiliko ambayo mimi ninaona ni ya kawaida tu,”alisema.

Mrage alijiunga na Kagera Sugar mwaka 2006 na kufanikiwa kuipa timu hiyo taji la Tusker na tangu hapo hawakuwahi kuchukua taji lolote.

Alisema anatafuta timu yoyote itakayomhitaji kwani ukocha ndio kazi anayotegemea katika maisha yake.

CHANZO: HABARI LEO

About Unknown

0 comments:

Powered by Blogger.