vilabu

NDANDA FC YAONYESHA NJIA YA KUREJEA DARAJA LA KWANZA, UKATA WAISUMBUWA


Wachezaji wa timu ya soka ya Ndanda FC ya mkoani hapa, wamegoma kufanya mazoezi kutokana na kutolipwa mishahara yao, wiki moja tu kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, msemaji wa timu hiyo, Idrissa Bandari, amesema hali hiyo inatokana na timu kukumbwa na ukosefu wa fedha na wapo wachezaji wanaodai mishahara ya miezi miwili na wengine mwezi mmoja.

“Tumeanza na ukata huu mapema sana msimu huu... kwasababu timu haina pesa na leo vijana hawajafanya mazoezi asubuhi na jioni hatuna mazoezi, vijana wanadai mishahara yao na sisi hatuna fedha, lazima tuwe wakweli," alisema na kuongeza:

"Tunapokwenda kupeleka barua sehemu za kuomba udhamini, ni ngumu sana kuenda mimi Idrissa au kiongozi wa Ndanda akapata zile fedha, lazima tupate sapoti ya mtu ambaye anaweza akaenda sehemu akazungumza na watu wakakubali kutokana na hadhi yake,” alisema.

Alisema benchi la ufundi limejitahidi kusajili wachezaji wazuri msimu huu ukilinganisha na msimu uliopita, lakini iwapo hali hiyo itaendelea, wananchi wa Mtwara wasitarajie makubwa kutoka kwa timu hiyo ambayo bajeti yake ni sh. Bilioni 1 kwa msimu nzima ingawa ikipatikana hata nusu yake inaweza kuwasaidia kuiendesha.

“Suala la mshahara ni suala kubwa sana na ni haki yao kudai, sisi kama tunapata Sh. milioni 500 leo tunaweza kuiendesha timu vizuri kabisa kwasababu tutakuwa tumeweza kutatua mahitaji yote muhimu... wachezaji asubuhi walieleza tu ukweli na kama binadamu au kama kiongozi inafikia hatua unaguswa na hoja zao... wana matatizo watayamalizaje nyumbani kwao?” Alisema.

Idrissa alisema, amelazimika kuzungumza hayo na vyombo vya habari ili wananchi wa Mtwara wafahamu kwamba bado timu yao ina matatizo na kwamba hawapaswi kulaumiwa kwa namna yeyote kwa matokeo au mwenendo nzima wa timu hiyo ukiwa tofauti na matarajio yao pindi ligi itakapoanza.

Aidha, ametowa wito kwa serikali ya mkoa na wadau wengine kujitolea kwa hali na mali kuisaidia timu, kwa kushawishi kampuni na mashirika mbalimbali yaliyopo mkoani humo kama ambavyo inafanyika katika mikoa ambayo ina kampuni za uwekezaji.

“Niwaombe sana watu wa Mtwara wenye nia na mapenzi mema na timu ya Ndanda... hali ya timu ni mbaya, na tusidanganyane kuiendesha timu kwa kuomba michango, timu ya ligi haiendeshwi hivyo, inaendeshwa kwa udhamini pamoja na bajeti yake ambayo inatengwa, lakini sisi hatuna hiyo fedha... hali ya Mtwara inajulikana, tuna kampuni nyingi, kama watu wanajitolea kutusaidia wale ambao wana nguvu na sauti zao zina nguvu, wakienda kwa watu kuwaona tunaweza kupata msaada mkubwa sana,” alisema.

CHANZO: NIPASHE

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.