TFF

TFF YAENDELEA KUPINDISHA KANUNI ZAKE KATIKA MCHEZO WA MTIBWA NA STAND


Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeendelea kuvunja kanuni zake lenyewe baada ya jana(juzi) kuruhusu mechi ya Mtibwa Sugar dhidi ya Stand United ichezwe asubuhi.

Mechi hiyo ya kwanza ya duru la pili kwa timu zote mbili, ilichezwa kwa dakika 45 za kwanza juzi (majuzi) kwenye Uwanja wa Manungu mkoani Morogoro kabla ya kipindi cha pili kumaliziwa jana asubuhi kutokana mvua kubwa iliyonyesha Turiani jumamosi jioni.

Goli la mabingwa wa 1999 na 2000 wa Tanzania Bara lilifungwa juzi na kiungo Mzamir Yassin katika dakika ya 22 ya mchezo.

Ushindi huo umekifanya kikosi cha Mecky Mexime kifikishe pointi 31 katika nafasi ya nne ya msimo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kikishinda tisa na kutoka sare mara nne.

Kuchezwa asubuhi kwa mechi hiyo ni kinyume cha Ibara ya 14 ya Kanuni za Ligi za TFF toleo la 2015 zilizopitishwa na Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo iliyoketi visiwani Zanzibar Juni 20 mwaka jana.

Kifungu cha 45 cha Kanuni hiyo kinasema: "Mchezo wowote wa Ligi Kuu unatakiwa kuchezwa kati ya saa nane mchana (1400hrs) na saa nne usiku (2200hrs)."

Msimu uliopita mechi za Mtibwa Sugar dhidi ya Kagera Sugar na Stand United na ile ya Stand United dhidi ya Kagera Sugar zililazimika kuchezwa asubuhi ya siku ya pili kutokana na viwanja vya Manungu na Kambarage kujaa maji.

Kifungu cha 48 cha Kanuni za Ligi za TFF kinaeleza kuwa ukiukwaji wa vipengele vyote vilivyopo katika Ibara ya 14 ya kanuni hizo, adhabu yake ni faini kati ya Sh. 200,000 hadi Sh. 3,000,000 na au kifungo cha mechi tatu hadi miezi mitatu.

CHANZO: NIPASHE (Februari 01, 2016)

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.