TFF

TFF YAITOZA SIMBA MILIONI 5


Kamati ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imeipiga faini ya sh. 5,000,000 (milioni tano) klabu ya Simba, kuiagiza ilipe gharama za uharibifu wa viti uliofanywa na washabiki wake katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya timu yake na Yanga iliyochezwa Oktoba Mosi mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pia Kamati hiyo katika kikao chake kilichofanyika jana (Oktoba 4, 2016), imelaani kitendo hicho na kuionya klabu hiyo kuwa vitendo vya aina hiyo vikiendelea itakabiliwa na adhabu kali zaidi ikiwemo kucheza mechi bila washabiki. Adhabu dhidi ya Simba imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 42(3) na 24(7) za Ligi Kuu.

Vilevile kwa kuzingatia Kanuni ya 9(8) ya Ligi Kuu, Kamati imefuta adhabu ya kadi nyekundu iliyotolewa na mwamuzi wa mechi hiyo kwa Jonas Mkude wa timu ya Simba baada ya kuthibitika bila mashaka kuwa nahodha huyo hakustahili kadi hiyo.

Mbali ya ripoti ya Kamishna na kupitia tena mkanda wa mechi hiyo iliyoonyeshwa 'live', Kamati inaendelea na uchunguzi wa jambo lingine kuhusu uchezeshaji wa mwamuzi wa mechi hiyo Martin Saanya, na wasaidizi wake Samwel Mpenzu na Ferdinand Chacha kabla ya kutangaza uamuzi wake.

Mkuu wa Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba, Haji Manara amepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa kuingia uwanjani baada ya mechi hiyo wakati yeye hakuwa miongoni mwa maofisa wa mechi waliotakiwa kuwepo katika eneo hilo.

Adhabu dhidi ya Manara ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(10). Eneo husika ni kwa ajili ya wachezaji, mabenchi ya ufundi, waamuzi, madaktari, huduma ya kwanza, wapiga picha na maofisa wengine wa mechi.

Klabu ya Azam imepigwa faini ya sh. 3,000,000 (milioni tatu) kwa kuvaa nembo ya mdhamini wa Ligi Kuu kwenye mkono mmoja tu badala ya miwili ambapo ni kinyume na Kanuni ya 13(1), na adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 13(6).

JKT Ruvu imepewa onyo na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya Msimamizi wa Kituo, na Ofisa wa Bodi ya Ligi kushambuliwa na mshabiki wa timu hiyo katika mechi dhidi ya Mbeya City iliyofanyika Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani. Mshabiki huyo amefungiwa miezi 12, na iwapo vitendo hicho vitaendelea Uwanja huo utafungiwa kwa mechi za Ligi Kuu.

Mwamuzi Ahmed Seif amefungiwa miezi sita kwa kushindwa kumudu mechi kati ya African Lyon na Mbao FC ikiwemo kutoa adhabu ya penalti ambayo haikuwa sahihi. Pia Mwamuzi huyo alipata alama za chini ambazo hazimruhusu kuendelea kuchezesha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom.

Pia Makamisha David Lugenge na Godbless Kimaro wamepewa onyo kwa kuwasilisha taarifa zenye upungufu katika mechi walizosimamia za raundi ya tano na saba.

Katika Ligi Daraja la Kwanza (FDL), Mbeya Warriors imepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa kupitia mlango usio sahihi ikiwemo kuvunja kufuli kwenye mechi kati yao na Kimondo FC iliyofanyika Septemba 24 mwaka huu Uwanja Vwawa mkoani Songwe. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(48) ya Ligi Daraja la Kwanza.

About dada

0 comments:

Powered by Blogger.