Na Ally Mohammed, Zanzibar.
Ligi kuu ya Zanzibar Grand Malt (ZGPL) imeendelea tena hii leo katika viwanja viwili vya Amaan mjini Unguja na Gombani Pemba.
UWANJA WA AMAAN
Klabu ya Bandari waliwavaa Mafunzo katika uwanja wa Amaani na mchezo huo kumalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1.
Bandari walikuwa wa kwanza kuliona lango la Mafunzo kupitia kwa mshambuliaji wao Mussa Omar 'Kidishi' katika dakika ya 25 na kuipeleka Bandari mapumziko wakiwa mbele kwa goli 1-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na iliwachukuwa dakika 7 tu Mafunzo kuweza kusawazisha kupitia kwa Mohammed Abdulrahim, na kupelekea mchezo kumalizika kwa sare ya goli 1-1.
UWANJA WA GOMBANI
Katika uwanja huo wa Gombani uliwashuhudia wawakilishi wengine wa Zanzibar katika michuano ya CAF, Jamhuri wakipokea kichapo cha goli 3-0 toka kwa Chipukizi.
Mabao ya Chipukizi yalifungwa na Muhsin Mohammed katika dakika ya 11 ya kipndi cha kwanza, bao la pili likifungwa na Faki Maalim katika dakika ya 21 ya kipindi cha kwanza, na kuipeleka mapumziko Chipukizi
wakiwa wanaongoza kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa Jamhuri kusaka magoli ya kusawazisha, huku Chipukizi wakitaka kuongeza, na alikuwa ni Faki Maalim kwa mara nyengine tena aliyeifungia Chipukizi bao la 3 katika dakika ya 60, na kupelekea mchezo kumalizika kwa Chipukizi 3 Jamhuri 0.
MICHEZO YA KESHO
Ligi hiyo inatarajia kuendelea tena kesho kwa mechi moja katika uwanja wa Amaan kwa kuzikutanisha timu za Mtende Rangers na Chuoni.
0 comments:
Post a Comment