Na Ally Mohammed, Zanzibar
Ligi kuu ya Zanzibar Grand Malt (ZGPL), jioni ya leo imeingia katika mzunguko wa pili kwa kushuhudia michezo miwili katika viwanja viwili tofauti.
UWANJA WA AMAAN
Katika kiwanja cha Amaan kisiwani Unguja, mabahari wa KMKM walikutana uso kwa uso na klabu ya Malindi.
Katika mechi hiyo iliyokuwa nzuri na ya kusisimua iliwachukuwa Malindi sekunde 57 kuandika bao la kwanza likitiwa kimiani na mshambuliaji wao Issa Hamad ambaye ameandika histotia kwa kufunga bao la mapema zaidi tangu ligi hiyo ianza wiki moja iliyopita.
Goli hilo lilidumu katika kipindi chote cha kwanza
na kuwapeleka mapumziko Malindi wakiongoza bao 1-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku KMKM wakifanya kila wanaloweza kukomboa bao hilo, na iliwachukua dakika mbili tu tangu kuanza kwa kipindi cha pili KMKM walisawazisha kupitia kwa Mudrik Muhib.
KMKM waliendelea kulisakama lango la Malindi na hatimae juhudi zao zikazaa matunda katika dakika ya 90 kufuatia bao la pili na la ushindi likifungwa na Maulid Kapenta.
GOMBANI, PEMBA
Huko kisiwani Pemba kwa mara nyengine tena mabingwa watetezi wa ligi hiyo, klabu ya Super Falcon ambao ni wawakilishi wa Zanzibar katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika walikubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Duma.
Mabao yote mawili ya Duma yalifungwa na Vuai Abdallah katika dakika ya 55 na 66, huku bao pekee la Super Falcon likifungwa na Mohammed Salum.
MICHEZO YA KESHO
Ligi hiyo itaendelea tena hapo kesho kwa michezo miwili, ambapo katika uwanja wa Amaan kisiwani Unguja, Mafunzo wataikaribisha timu ya Bandari iliyopanda daraja msimu huu, na huko kisiwani Pemba, Chipukizi watacheza na washindi wa pili wa ligi iliyopita klabu ya Jamhuri ambao wana tiketi ya kushiriki kombe la Shirikisho hapo mwakani, mechi itakayochezwa katika uwanja wa Gombani.
0 comments:
Post a Comment