BUSHIRI AZISHUKURU SIMBA NA YANGA

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya KMKM ya Zanzibar Ali Bushir amesema mechi za kirafiki kati ya Simba na Yanga zimemsaidia kubaini mapungufu makubwa katika kikosi chake na hivyo anajipanga kukitengeneza ili kufanya vizuri kwenye Kombe la Mapinduzi.

Akizungumza na gazeti hili, Bushir alisema baadhi ya mapungufu aliyoyagundua yapo katika safu za ushambuliaji, ulinzi na kiungo.

“Nashukuru kwamba mechi hizi zimenifanya nigundue makosa mengi katika kikosi changu lakini sasa, nataka kuboresha kwa sababu timu hizi tutakutana nazo katika Kombe la Mapinduzi na nia ya kila mmoja wetu ni kuchukua ubingwa, nitayarekebisha makosa yasiweze kujirudia,” alisema.

Bushir alisema KMKM ina kibarua kizito mbele hasa kwa vile inatarajia kushiriki michuano ya kimataifa mwakani. KMKM ilicheza na Yanga Jumamosi na kuambulia kipigo cha mabao 3-2, kabla ya kuchapwa na Simba mabao 3-1 Jumapili.

Alisema kwa jinsi alivyoona timu zote mbili amegundua ni nzuri na zina wachezaji wazuri ingawa anasema hakuona baadhi ya wachezaji wake nyota hasa upande wa Yanga.

Kwa mujibu wa Bushir, wachezaji wake hawana uelewa na uzoefu wa kutosha dhidi ya mechi kubwa kama hizo ndio maana walifanya vibaya.

“Timu yetu haina welewa wa kutosha wala uzoefu na mechi hizi, ninawaambia mashabiki waondoe hofu juu ya kufungwa kwetu tutaboresha mapungufu yote kusudi tufanye vizuri wakati ujao,” alisema.


CHANZO: HABARI LEO

0 comments:

Post a Comment

Powered by Blogger.