MANISPAA WAKWAMIDHA UJENZI WA JANGWANI CITY

UONGOZI wa klabu ya Yanga, umesema Manispaa ya Ilala inakwaza mchakato wa ujenzi wa uwanja mpya wa kisasa wa klabu hiyo unaotarajiwa kujengwa ulipo wa zamani wa Kaunda ambao baada ya kukamilika utaitwa Jangwani City.

Yanga ilianza mchakato huo wa ujenzi wa uwanja miezi kadhaa iliyopita na kufanikiwa kupata ramani iliyoandaliwa na Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group Ltd waliojenga Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu, alisema jana kwamba hadi sasa wao wanasubiri majibu kutoka Manispaa ya Ilala ili waweze kuanza mchakato huo wa ujenzi.

Alisema mara ya mwisho manispaa waliwataka kukagua mipaka yao na kuwasilisha kwao, na walifanya hivyo, lakini hadi sasa bado hawajapata jibu lolote kutoka kwao, hivyo kukwaza mchakato wa ujenzi huo ambao kama si vikwazo hivyo ulipaswa uwe umeanza.

“Unajua kila kitu na mipango, sisi tunafanya mambo kwa taratibu na ndiyo maana walivyotuambia tukague mipaka tulifanya hivyo na kuwapelekea, ila hadi sasa bado hawajatujibu,” alisema na kuongeza kuwa wanawasubiri wao.

Sakata la ujenzi huo wa uwanja wa Yanga katika eneo la Jangwani, lilizua sintofahamu kutokana na wakazi wa eneo hilo kugoma kuondoka kwa madai wao ni wamiliki halali wa eneo hilo, huku wengine wakihoji sababu za wao kutaka kuhamishwa kwenda Mabwepande huku Yanga wakiruhusiwa kufanya ujenzi.

Juhudi za kumpata Ofisa Habari wa Manispaa ya Ilala, Tatu Shaibu kuzungumzia suala hilo, zilishindwa kuzaaa matunda kutokana na kutopatikama kupitia simu yake ya kiganjani.


CHANZO: TANZANIA DAIMA

0 comments:

Post a Comment

Powered by Blogger.