ASHANTI WABANWA, MBEYA CITY WAKICHAPWA

Timu za Ashanti United na Spice Stars ya Unguja leo zimetoshana nguvu baada ya kutoka sare ya goli 1-1 katika mchezo wa kuwania kombe la Mapinduzi ULIKOPIGWA Uwanja Amaan.

Ashanti ndiyo walikuwa wa kwanza kuandika goli katika dakika ya 22 kupitia kwa Ike Brighton raia wa Nigeria ambaye alipachika goli maridadi kutoka pembezoni mwa lango kufuatia kuingia ndani ya eneo la hatari kwa kasi na kuachua mkwaju wa juu kwa mguu wa kulia uliomshinda mlinda lango wa Spice Mohamed Silima.

Wauza mitumba hao wa Ilala Dar es Salaam wangeweza kuongeza la pili dakika nne baadaye pale Brighton alipmramba chenga Silima lakini Laurent Mugia akawa mzembe kuunganisha mpira langoni.

Kipindi cha pili kilikuwa cha Spice ambao walicharuka na kulishambulia lango la Ashanti kwa nguvu na jitihada zao zilizaa matunda dakika ya 80 pale Abdallah Seif Bausi aliposawazisha kwa mpira wa kichwa ambao mlinda lango Juma Mpongo alishindwa kuudhibiti mikononi.

Na kama si uimara wa Mpongo langoni basi Spice wangeweza kuondoka na ushindi kwa wachezaji wake hasa Yunus Roma walipoteza nafasi tatu muhimu za kupachika magoli.

AZAM WATINGA ROBO

Mabingwa watetezi wa kombe la Mapinduzi, Azam FC wamefanikiwa kutinga robo fainali ya michuano hiyo baada ya kuwachapa makamu bingwa wa mwaka jana Tusker ya Kenya kwa goli 1-0 katika mchezo mkali ulipigwa uwanja wa Amaan usiku huu na kumalizika muda mfupi uliopita.

Goli pekee katika mchezo huo lilitiwa kimiani kwa ufundi wa hali ya juu na mshambulaji Kipre Tchetche raia wa Ivory Coast dakika moja kabla ya mapumziko pale alipopokea pasi murua ya kiungo Himid Mao akiwa pembeni kushoto mwa eneo la hatari kisha akawapiga chenga walinzi watatu waliokuwa wamemzunguka na kuachia mkwaju mkali kwa guu la kushoto uliotinga kimiani upande wa juu kulia mwa lango la Tusker na kumwacha mlinda lango Samuel Odhiambo akiwa ameduwaa licha ya kuchupa kwa juhudi kubwa.

Matokeo yake Tusker wanaofundishwa na kocha wa zamani wa Harambee Stars, Francis Kimanzi walijikuta wakichezewa nusu uwanja kwa muda mrefu kipindi cha kwanza na walijitahidi kurejea mchezoni kipindi cha pili wakitumia mipira mirefu na mipira ya kurusha ya Luke Ochieng lakini juhudi zao ziliishia patupu.


Huko Pemba URA wamewanyanyasa wenyeji Clove Stars kwa kuwachapa magoli 3-1 wakati Mbeya Simba wamekiona cha moto kwa kukubali kichapo cha magoli 2-1 kutoka kwa wenyeji Chuoni.

0 comments:

Post a Comment

Powered by Blogger.