TFF LEO; ITC ya Mganda wa Mtibwa yatua, Ngao ya Jamii sep11

Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Uganda (FUFA) limetuma Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa ajili ya mchezaji Ayoub Hassan Isiko aliyejiunga na Mtibwa Sugar akitokea timu ya Bull FC ya nchini humo.

ITC hiyo ilitumwa jana (Agosti 30 mwaka huu), hivyo kufanya wachezaji ambao ITC hazijapatikana hadi sasa kubaki wawili tu.

Dirisha la usajili wa wachezaji litafungwa rasmi Septemba 4 mwaka huu. Wachezaji ambao ITC zao bado hazijapatikana ni Salum Kinje na Pascal Ochieng kutoka AFC Leopards ya Kenya waliojiunga na Simba.

ITC hizo zinatarajiwa kupatikana wakati wowote kwani tayari Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeshaziomba kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF) baada ya nyaraka zote zilizokuwa zikitakiwa kupatikana.


WACHEZAJI 17 WAWEKEWA PINGAMIZI

Klabu mbalimbali zimewasilisha pingamizi Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupinga usajili wa wachezaji 17 walioombewa usajili katika timu za Ligi Kuu.

Toto Africans ya Mwanza imewawekea pingamizi wachezaji Enyinna Darlinton aliyeombewa usajili Kagera Sugar, na Mohamed Soud anayekwenda Coastal Union kwa maelezo kuwa bado ina mikataba na wachezaji hao.

Pia Flamingo ya Arusha inapinga usajili wa wachezaji wake Kelvin Friday Iddy katika timu za Azam na Salim Walii (Polisi Mara) kwa vile taratibu za kuwahamisha bado hazijafanywa.

Nayo Kagera Sugar inapinga usajili wa beki David Charles Luhende kwenda Yanga kwa vile ada ya uhamisho haijalipwa.

Super Falcon ya Chanjamjawiri, Chakechake, Pemba inapinga wachezaji wake wanne; Edward Christopher Shija, Samir Said Luhava (Simba), Robert Joseph Mkhotya (African Lyon) na Sultan Juma Shija (Coastal Union) kusajiliwa katika timu hizo kwa maelezo taratibu halali za uhamisho hazikufuatwa.

Mchezaji Othman Hassan aliyeombewa usajili Coastal Union anapingwa na Oljoro JKT kwa vile bado ana mkataba na timu hiyo unaomalizika Mei 24, 2013. Nayo Rollingstone Multipurpose Ateclass Foundation ya Arusha inapinga usajili wa Kigi Makassy kutoka Yanga kwenda Simba hadi itakapolipwa fidia ya kumlea mchezaji huyo kwa vile bado hajafikisha umri wa miaka 23.

Azam inapinga usajili wa Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kwenda Simba kwa maelezo bado ina mkataba naye unaomalizika Juni 11 mwakani. Nayo Simba inapinga Kelvin Yondani kusajiliwa Yanga kwa maelezo kuwa ina mkataba naye uliosainiwa Desemba 23 mwaka jana.

Vilevile Simba imewasilisha malalamiko ya mchezo usio wa kiungwana katika usajili wa Mbuyu Twite aliyeko Yanga kwa maelezo alisaini mkataba na klabu yao Agosti Mosi mwaka huu mbele yao, viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Rwanda (FERWAFA) na APR ambapo alilipwa dola 30,000 na nyingine 2,000 ikiwa ni fedha ya kujikimu na nauli yake ya kujiunga na klabu hiyo.

Nayo Yanga inapinga Simba kuwaacha wachezaji Dan Mrwanda, Haruna Shamte, Kanu Mbiyavanga na Lino Masombo kwa maelezo walishapatiwa leseni za kucheza Ligi ya Tanzania walizozitumia kwenye mashindano ya Kombe la Kagame.

Pia inapinga Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kujiunga Simba kwa vile ana leseni ya kuchezea Azam kwa msimu wa 2012/2013.

Pingamizi lingine la Yanga kwa Simba ni
kuwa imezidisha idadi ya wachezaji wa kigeni wanaotakiwa kusajiliwa kwa maelezo inao wanane wakati wanaoruhusiwa ni watano. Imewataja wachezaji hao kuwa ni Lino Masombo, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Mussa Mude, Kanu Mbiyavanga, Pascal Ochieng, Komalmbil Keita na Daniel Akuffor.

Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa inatarajia kukutana Jumapili (Septemba 2 mwaka huu) kupitia pingamizi hizo pamoja na usajili wa wachezaji kwa ujumla kwa 2012/2013.


SIMBA Vs AZAM SEP 11

Mechi ya Ngao ya Jamii (Community Shield) kuashiria ufunguzi rasmi wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2012/2013 kati ya bingwa mtetezi Simba na makamu bingwa Azam itachezwa Septemba 11 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Awali mechi hiyo ilipangwa kupigwa Septemba 8 katika uwanja huo.


SERENGETI BOYS KUJIPIMA KWA ASHANTI

Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) iliyokuwa kambini kujiandaa kwa mechi dhidi ya Kenya itavunja rasmi kambi yake kesho (Jumamosi) kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Ashanti United.

Mechi hiyo dhidi ya Ashanti United iliyoko daraja la kwanza itachezwa kuanzia saa 10 jioni Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kwa kiingilio cha sh. 2,000.

Serengeti Boys ilikuwa Septemba 9 mwaka huu icheze na Kenya kwenye mechi ya raundi ya kwanza ya michuano ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17, lakini Kenya ikajitoa ambapo sasa itacheza na Misri katika raundi ya pili. Mechi ya kwanza itachezwa Oktoba 14 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Mwishoni mwa Septemba, Serengeti Boys itarejea tena kambini kujiandaa kuikabili Misri ambapo kabla inatarajia kupata mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya timu itakayotangazwa baadaye.

0 comments:

Post a Comment

Powered by Blogger.