
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’, Salum Bausi anatarajiwa kuingia mkataba kufundisha timu ya Taifa ya Sudan Kusini.
Hayo yamebainishwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya ZFA Taifa, Hashim Salum alipokuwa akizungumzia juu ya ukweli wa taarifa hiyo kuhusu kocha huyo.
Salum, ambae alikuwa meneja katika kikosi cha Zanzibar Heroes kilichoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji iliyofanyika Kenya, alithibitisha suala hilo na kusema kuwa kabla ya kusaini mkataba huo ataletewa kwanza ausome na kuuelewa kabla ya kufikia makubaliano.
Alisema kuwa juzi usiku alipata simu kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka nchini Sudan Kusini kumjulisha juu ya makubaliano na kocha huyo.
“Walinipigia simu na kunijulisha yale yote yaliyojiri baina ya kocha wetu huyu, na kuniarifu kwamba wakati wowote wataleta mfano wa mkataba ili auone kocha na kama atakubaliana makubaliano yaliyomo atajaza na kwenda Sudan kuifundisha timu hiyo,” alisema.
Alisema kuwa sababu iliyowafanya nchi hiyo kumtaka Bausi afundishe timu yao ni kutokana na kuwachambulia kwa kina juu ya uwezo wa timu hiyo kutokana na kiwango walichoonesha tangu mwaka jana kwenye michuano hiyo na kuweza kuwapa maelekezo ambayo iwapo watayafuata kwa kiasi kikubwa wataweza kufanikiwa.
Alisema, mpango huo unakwenda vizuri na kilichobakia ni Wazanzibari kumuombea dua ili aweze kufanikiwa mipango yake. Awali, alipowasili mjini hapa kutoka Kenya kwenye michuano ya Chalenji ambapo timu yake iliishia kwenye makundi safari hii, Bausi alisema kuwa amepata nafasi hiyo na hana sababu ya kuikataa.
CHANZO: HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment