CECAFA

KILIMANJARO WATWAA UBINGWA WA CECAFA


Haikuwa ubashiri, badala yake ilikuwa ni mipango thabiti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuhakikisha kwamba inavuna ushindi na kuwa mabingwa wa Kombe la Chalenji la CECAFA kwa wanawake baada ya kuilaza Kenya mabao 2-1 katika mchezo wa fainali uliofanyika Uwanja wa Nambole jijini Jinja nchini Uganda.

Mabao ya timu ya taifa Tanzania ya wanawake maarufu kama Kilimanjaro Queens katika mchezo wa leo Septemba 20, 2016 yamefungwa na Mwanahamisi Omari katika kipindi cha kwanza kabla ya Kenya kujitutumua na kupata bao la kufutia machozi kipindi cha pili katika mchezo uliokuwa na ushindani wa aina yake.

Matokeo hayo yatakuwa kupozwa kwa ndugu zao wa Zanzibar Queens ambao walitolewa mapema katika mashindano hayo yaliyoanza Septemba 11, 2016 kabla ya kufikia tamati leo katika fainali hizo zilizovutia mashabiki wa mpira wa miguu nchini Uganda ambako kila upande ulikuwa na watu wanaowasapoti.

Timu hiyo inatarajiwa kuondoka nchini Uganda kesho Jumatano na kwenda moja kwa moja Kagera ambako ilipiga kambi kabla ya kwenda Jinja. Itarudi hapo kusema ahsante kwa wenyeji, lakini pia kuwapa pole ya janga la Tetemeko la Ardhi wakazi lililotokea katika mikoa huo na mikoa jirani ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani. Mikoa ambayo iliathirika zaidi ni Kagera na Mwanza kadhalika nchi jirani za Uganda na Rwanda.

Mara baada ya kuwapa pole, timu hiyo itasafiri kutoka Kagera kwa usafiri wa anga ambako taratibu za safari hiyo zitatangazwa na TFF hapo kesho ambako wananachi watapata fursa ya kuipokea na kuishangilia timu hiyo inayonolewa na Kocha Sebastina Nkoma akisaidiuwa na Hilda Masanche wakiwa chini ya Mwenyekiti wa soka la wanawake.

Safari ya ubingwa wa Kilimanjaro Queens ulianzia hatua ya makundi kwa kuilaza Rwanda manbao 3-2 kabla ya kutoka sare tasa na Ethiopia ambayo pia ilivuna ushindi wa mabao 3-2 kutoka kwa Rwanda. Tanzania na Ethiopia zilitoka sare na kurusha sarafu ambako Tanzania ikawa ya kwanza katika kundi B hivyo kucheza na Uganda ambayo ililala kwa mabao 4-0 katika mchezo wa nusu fainali. Na leo Septemba 20, 2016 ikatawazwa kuwa mabingwa kwa ushindi wa mabao 2-1.

Timu zote shiriki zilikuwa Tanzania, Burundi, Zanzibar, Kenya, Ethiopia, Rwanda pamoja na mwenyeji Uganda. Mashindano ya Kombe la Chalenji la CECAFA kwa timu za wanawake yamefanyika kwa mara ya kwanza jambo linaloleta tafsiri kuwa michuano hiyo inaweza kuinua soka la wanawake kwa ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.