CECAFA

KILI STARS MDOMONI MWA UGANDA ROBO FAINALI YA KWANZA

Timu ya taifa ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' leo  watakuwa na kibarua mbele ya Uganda katika robo fainali ya kwanza ya kombe la chalenge inayo endelea nchini Kenya.

Kilimanjaro Stars imefika hatua hiyo baada ya kushika nafasi ya pili katika Kundi la B lililokuwa na timu za Zambia, Burundi na Somalia. Zambia ambayo ni timu mwalikwa, iliongoza kundi hilo.

Bara itashuka dimbani ikifahamu kuwa ina kazi kubwa ya kukabiliana na Uganda ambao ni mabingwa watetezi, na waliofika hatua hiyo kwa kushinda mechi zake zote tatu za Kundi C.

Hata hivyo, kikosi cha Kocha Kim Poulsen kinajivunia wachezaji mahiri ambao ni mchanganyiko wa yosso pamoja na wazoefu ambacho kimeonesha kucheza kitimu tangu mechi ya kwanza na Zambia waliyokwenda nayo sare na dhidi ya Somalia na Burundi ambazo walizifunga bao 1-0 kila moja.

Ivo Mapunda ndiye kipa tegemeo na ameonesha kiwango kizuri katika mechi zote tatu, akionesha uzoefu kwa kulinda lango vyema, huku akisaidiwa na mabeki Himid Mao, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani na Said Morad, lakini kiungo kikiwategemea Salum Abubakar, Frank Domayo, Athumani Chuji, Ramadhan Singano.

Katika ushambuliaji, Kim anajivunia nyota wawili wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu, pamoja na Mrisho Ngasa, Haruna Chanongo na Amri Kiemba.

Hata hivyo, Kili Stars inapaswa kuwa makini na Uganda ‘The Cranes’ kwani inao wachezaji mahiri wakiongozwa na nahodha Emmanuel Okwi, Hamis Kiiza, Dan Sserunkuma, Godfrey Kizito na Muddie Kagere, ambao wameonesha soka ya hali ya juu chini ya kocha Sredojevic Milutin ‘Micho.’

Akizungumza jana Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Boniface Wambura alisema wameweka nguvu kubwa katika timu hiyo kuhakikisha inafanya vyema ili kunyakua ubingwa au nafasi ya pili.

“Tuna msafara wa watu karibu 33 wakiwemo wajumbe wawili wa Kamati ya Utendaji ya TFF, hiyo ni tofauti na miaka ya nyuma. Lengo letu ni kuhakikisha Kilimanjaro inacheza fainali na kuchukua ubingwa ikishindikana basi hata nafasi ya pili,” alisema Wambura.

Alisema anajua Bara inakutana na timu ngumu ya Uganda iliyowatoa kwenye hatua ya nusu fainali mwaka jana, lakini kwa mujibu wa kocha Kim, hilo hawalihofii kutokana na kikosi alichokuwa nacho.

“Kocha ametuambia kikosi chake kipo vizuri maandalizi kwa ajili ya mchezo huo yamekamilika na hana majeruhi,” alisema Wambura.

Baada ya mechi ya Kilimanjaro Stars dhidi ya Cranes itakayoanza saa 8 kamili mchana, wenyeji Kenya wataikabili Rwanda saa 10 jioni. Mechi za mwisho za robo fainali zitafanyika kesho.



RATIBA YA MICHEZO YA ROBO FAINALI ZA CHALLENGE

Desemba 7, 2013;
Uganda   VS Tanzania (Saa 8:00 Mchana)
Kenya   VS Rwanda (Saa 10:00 Jioni)

Desemba 8, 2013
Zambia   VS   Burundi (Saa 8:00 Mchana)
Ethiopia  VS  Sudan (Saa 10:00 Jioni)

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.