
WAKATI ikiwa si shwari ndani ya klabu ya Simba, hatimaye Mwenyekiti wake, Ismail Aden Rage ‘Tutu Vengere’ jana aliibuka jijini Dar es Salaam na kujinasibu kuwa yeye ni ‘mwanaume wa mbegu’ klabuni Msimbazi.
Rage, aliyepewa jina la Tutu Vengere na mashabiki wake, likiwa na maana ya mtu mwenye msimamo mkali, amezidi kuwachanganya wanachama wa klabu hiyo, ambao wamekuwa wakizungumza maneno makali ya kumtaka kuondoka ndani ya klabu hiyo na hali ilizidi kuwa mbaya baada ya juzi watani wao Yanga kuanika hadharani kuwa wamemnasa aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi.
Mwenyekiti huyo, jana asubuhi aliibuka katika kilinge cha wadau wa soka kilichoko jirani na Idara ya Habari (Maelezo), Posta Mpya jijini, huku akitamba kuwa hakuna mtu anayemuogopa, kwani amekamilika kila idara na kwamba amerejea kwa kishindo baada ya kutoonekana kwa muda.
Huku wadau wengine wa soka wakimsikiliza kwa makini, akiwamo mwanachama wa Yanga ajulikanaye kwa jina maarufu la Makaranga, alisema kuwa, yeye amerejea na huenda akatoa neno lake la moyoni kuhusu hali inavyoendelea ndani ya Simba hivi sasa.
Rage alidai kuwa yeye ana umuhimu mkubwa ndani ya klabu hiyo na ndio maana jana, viongozi walimpigia simu kutoka Zanzibar walikoweka kambi kwa ajili ya mchezo wa Jumamosi wa Mtani Jembe dhidi ya Yanga, wakimwambia kuwa hawana fedha.
“Hapa nilipo nimepigiwa simu kutoka kambini Zanzibar, timu haina hela, ndio nashughulikia ili nimuite Katibu Mkuu awapelekee huko,” alitamba Rage na kuongeza kuwa wanachama wa Tawi la Mpira Pesa na mashabiki waendelee kupiga kelele, lakini mwanaume ameshatua na timu inahitaji huduma zake.
Rage alienda mbali zaidi na kupasha kuwa ndani ya klabu ya Simba hakuna mtu anayejitolea kama yeye na Zakaria Hanspope na kuwa anawashangaa wanaopiga porojo wakati hawana mchango wowote katika uendeshaji wa timu hiyo.
Aidha, kuthibitisha kishindo cha ujio wake, Rage jana jioni alitinga Makao Makuu ya Simba, na kuzungumza na wanachama na mashabiki kiduchu waliokuwepo hapo, huku baadhi wakimhoji maswali juu ya aliyekuwa mshambuliaji wao Emmanuel Okwi, ambaye amenaswa na Yanga.
Mmoja wa wanachama waliokuwepo klabuni, Mgeni Ramadhan ‘Macho’, aliipasha Tanzania Daima kuwa Rage aliulizwa juu ya fedha alizouzwa Okwi na kujibu kuwa ana mpango wa kusaka wanasheria ili wasimamie suala hilo na klabu yao hiyo iweze kulipwa fedha hizo.
“Rage alisema kitu kikubwa kilichofanya Okwi aende Yanga ni hujuma kutoka kwa watu ndani ya klabu, huku akisema, Kamati ya Usajili ndiyo chanzo kikubwa cha Okwi kwenda Yanga,” alisema Macho akimkariri Rage.
Juhudi za Tanzania Daima kumpata Rage kuzungumzia suala hilo la Okwi baada ya kuongea na baadhi ya wanachama ziligonga mwamba, ambako simu yake ya kiganjani haikupatikana kila ilipopigwa.
Vivyo hivyo kwa upande wa Hanspope ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, ambaye juhudi za kumsaka kujibu tuhuma hizo zilishindikana.
CHANZO: TANZANIA DAIMA
0 comments:
Post a Comment