MSAFARA wa wachezaji na viongozi wa timu ya taifa ya wanawake chini miaka 20 ‘The Tanzanite’ unatarajiwa kuondoka nchini leo kwa ndege ya Fast Jet kwenda Afrika Kusini kwa mechi ya marudiano dhidi ya wenyeji wao Basetsana, itakayopigwa Jumamosi hii.
Msafara huo wa wachezaji 21 na viongozi sita, unaongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutokea Kanda ya Tanga na Kilimanjaro, Khalid Mohammed.
Tanzanite ilikabidhiwa bendera ya Taifa na Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Boniface Wambura na kupokelewa na nahodha wake Fatuma Issa, aliyewataka Watanzania kutokatishwa tamaa na matokeo ya mechi ya kwanza, badala yake wawaombee.
Fatuma alibainisha kuwa, matarajio yao ni kupata ushindi ugenini dhidi ya Afrika Kusini, ambako watapigana kadri wawezavyo kufanikisha hilo, hasa baada ya kuzifanyia kazi kasoro zilizowaangusha nyumbani na kuchapwa mabao 4-1.
“Watanzania wote wanapaswa kutuamini, kutusapoti na kutotukatisha tamaa. Sisi kama wachezaji tunahitaji sana hivyo vitu kutoka kwao ili kutuwezesha kufikia lengo la kuwang’oa wapinzani wetu na kusonga hatua ijayo,” alisema Fatuma.
Kwa upande wake kocha Rogasian Kaijage, alisisitiza kuwa, soka ingali katika falsafa yake ya muda mrefu kuwa, ni mchezo wa makosa, hivyo watahakikisha hawafanyi makosa na kuwa makini katika kuyatumia yale yatakayofanywa na wapinzani wao.
“Tukiangalia kilichotokea hapa wakati wakitufunga mabao 4-1, tutagundua na kukubaliana na ukweli kuwa hawakutuelemea, bali walikuwa makini kutumia makosa yetu vizuri. Tumejifunza na kufanyia kazi hilo, tunaamini tunaweza kufanya vema,” alisema Kaijage.
Katika pambano la awali lililofanyika jijini Dar es Salaam, Tanzanite ilikubali kichapo cha mabao 4-1, hivyo kuzua hofu miongoni mwa Watanzania kama inaweza kuyabadili matokeo hayo ugenini na kufuzu raundi ya tatu kuwania fainali za Dunia kwa vijana.
Kama itafanikiwa kuwatoa Basetsana, Tanzanite itafuzu raundi ya tatu na ya mwisho ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia kwa wanawake chini ya miaka 20, zitakazofanyika mwakani nchini Canada.
0 comments:
Post a Comment