
MARCIO Maximo. Alikuja nchini akiwa mtu wa kawaida. Baadaye kwa wajanja akageuka shujaa. Kwa wenye mtazamo wa karibu akageuka kuwa adui. Wakati anaondoka nchini akaonekana mjinga. Muda si mrefu pande zote mbili zikamuona alifaa. Nasikia anataka kurudi tena nchini kama shujaa.
Nasikia anakuja kujiunga na Yanga. Hakuna tatizo
katika hilo. Yanga imara ndio Taifa Stars imara. Simba imara ndio Taifa
Stars imara. Azam imara ndio Taifa Stars imara. Mbeya City imara ndio
Taifa Stars imara.
Unaposikia kocha kama Maximo anakuja kufundisha
timu kama Yanga hakuna unachoweza kufanya. unasubiri kwa hamu. Unalamba
midomo kwa matamanio. Unajua tunaweza kuzalisha akina Jerry Tegete
wengine. Akina Kiggi Makasi wengine.
Lakini upande wa pili wa kichwa unaanza kujiuliza maswali.
Waliomchukua Maximo wanamfahamu vizuri? Wanajua
kwa nini alizalisha wachezaji kama akina Tegete? Jibu ni rahisi tu. Ni
kwa sababu ya kiburi chake. Kiburi cha kuwaamini wachezaji chipukizi na
msimamo wake wa kutoyumbishwa na wachezaji tunaowaona mastaa.
Kama Yanga wakiamini katika kiburi chake, Maximo
atawafaa sana, hasa katika mechi za kimataifa na kuitengeneza timu imara
ya kesho na keshokuwa. Kama Yanga hawataamini kiburi chake, basi hakuna
walichofanya katika kumleta Maximo. Ni bora wangemwacha huko huko.
Mtu aliyemleta na kumlipa, Rais Jakaya Mrisho
Kikwete alimwacha afanye kazi yake. Rais wa TFF iliyopita, Leodeger
Tenga alimuacha afanye kazi yake. Swali linakuja kwa Yanga kama wanaweza
kumwacha afanye kazi yake.
Kuna mfano mdogo tu wa mchezaji kama Emmanuel
Okwi. Huyu ni staa sana katika soka letu. Lakini ameitumikia Yanga
katika mechi chache sana tangu asajiliwe kwa uhamisho wa pesa mbaya
kutoka Uganda.
Inadaiwa kuwa Okwi aligoma kucheza Yanga kwa
sababu alikuwa hajalipwa pesa zake. Katika kesi kama hii, Maximo atakufa
na viongozi wa Yanga kwa sababu hawezi kukubali kumkosa staa wake kwa
sababu nyepesi kama hii.
Lakini kuna kesi ya pili. Wakati fulani Okwi
anaweza kutimiziwa kila kitu na viongozi wake. Lakini bado anaweza
kubaki nchini kwao kwa siku nyingi zaidi.
Hii sio kwa Okwi tu, bali hata kwa Hamis Kiiza ‘Diego’ na wachezaji wengi wengine wa kulipwa wa klabu mbalimbali nchini.
Viongozi watamwacha Maximo ashughulike nao
wachezaji wa namna hii? Uamuzi wake wanaweza kuwa wa mwisho? Mara zote
wachezaji wa namna hii wanachelewa, lakini unakuta viongozi wa klabu
wanawapokea pale Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNI)
kama Wafalme tena huku wakijigamba katika vyombo vya habari.
Wachezaji wetu hawana nidhamu kwa sababu wanamtumikia mtu aliyewasajili na hawamtumikii kocha wala klabu.
Mfumo huu haupo Taifa Stars na ilikuwa rahisi kwa Maximo kufanya kazi yake kwa sababu aliweka pamba masikioni.
Vinginevyo kama Yanga wakiishi vizuri na Maximo,
kama atakuja, ana nafasi nzuri ya kuubadili mtazamo wa klabu kuhusu
falsafa ya kuipeleka Yanga mbele.
Ni mzuri pia katika masuala ya utawala kama vile masuala ya udhamini, maandalizi ya mazoezi, mikataba ya wachezaji na mengineyo.
Itatetegemea Yanga wameongea nini na Mbrazil huyu.
Kama waliongea kuhusu mshahara wake tu bila mengineyo, hapana shaka
maisha yake Jangwani yanaweza yakajaa filamu nyingi za kusisimua.
0 comments:
Post a Comment