gofu

Tanzania yatokota gofu Malawi

TANZANIA imeshindwa kujishikilia kwenye michuano ya gofu ya Kanda ya Sita Afrika iliyomalizika kwenye viwanja vya klabu ya Lilongwe, Malawi.

Kwa mujibu wa Ofisa Tawala wa Chama cha Gofu Tanzania (TGU), Sophie Nyanjera, Tanzania ambayo ilianza vema siku mbili za mwanzo imeshindwa kutamba na kujikuta ikimaliza nafasi ya 7 kati ya nchi 10 zilizoshiriki.

Tanzania ambayo mwaka 2011 ilishika nafasi ya tatu kwenye michuano iliyofanyika Mombasa, Kenya ilimaliza kwenye nafasi ya 7 baada ya kukusanya pointi 11 katika raundi nne.

Walianza vema siku ya kwanza kwa kukusanya pointi 4.5 za mechi za mchezaji mmoja mmoja (single matchplay) kati ya mechi nane zilizochezwa na kukusanya pointi 5 katika foursomes na better ball (mechi za wawili wawili) siku ya pili hivyo, kupanda hadi nafasi ya pili wakiwa na pointi 9.5.

Lakini timu hiyo, imeshtua wengi baada ya kupata pointi 1.5 pekee katika raundi ya mwisho ya single matchplay katika mechi nane.

Nahodha Frank Roman alishinda mechi yake dhidi ya Clive Zulu wa Zambia na John Saidi kutoka sare Clive Nguru wa Zimbabwe kwenye raundi hiyo, huku Abbas Adam, Jonh Leonce, Elisante Lembris, Nuru Mollel, Michael Makala na Jimmy Mollel wote wakipoteza mechi zao.

Timu hiyo ambayo iliondoka Jumamosi kwa basi chini ya kocha mkuu mchezaji wa kulipwa nchini Olais Mollel na meneja Richard Gomes inatarajia kuwasili leo.

Katika michuano hiyo mabingwa watetezi Afrika Kusini wameendelea kutamba kwa kuibuka mabingwa wakikusanya pointi 22.5 na kufuatiwa na Namibia wenye pointi 15, wakati Kenya ambao walikuwa nafasi ya tano wakikusanya pointi 5.5 siku mbili za mwanzo za michuano walizinduka na kukusanya pointi 13.5 na kushika nafasi ya tatu.

Hata hivyo, Kenya ambao ni mabingwa wa mwaka 2011 na mwaka jana kushika nafasi ya pili wameshuka. Wenyeji Malawi wamemaliza nafasi ya nne pointi 13 sawa na Zimbabwe ambao wapo nafasi ya tano, Uganda ambao walianza katika nafasi ya pili walijikuta wakitupwa nafasi ya sita pointi 12.5.

Matokeo ya timu nyingine Zambia nafasi ya nane 8.5, Msumbiji tisa 6.5, na Mauritius walimaliza mkiani wakiwa na pointi 4.5.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.