basketball

11 WAJITOKEZA KWANIA KUONGOZA KIKAPU

WAKATI uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) ukiwa katika hati hati ya kutofanyika wagombea 11 wamejitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali huku nyingine zikiwa hazina wagombeaji waliojitokeza.

Awali, uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Desemba 10, jijini Mbeya lakini ukaahirishwa hadi Desemba 28, kutokana na sababu mbalimbali na kubwa likiwa idadi ya wagombea kuwa ndogo na ukosefu wa fedha za kuendeshea uchaguzi wenyewe.

Tarehe ya mwisho wa kuchukua fomu ilikuwa jana. Hata hivyo, Rais wa TBF Mussa Mziya alisema kuwa uchaguzi huo utafanyika ikiwa kutapatikana fedha.

Akizungumza na gazeti hili kuhusu idadi ya wagombea, Ofisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Richard Mganga alitaja nafasi zinazowaniwa katika uchaguzi huo ni Rais ambapo wamejitokeza wagombea wawili, Makamu wa Rais amejitokeza mmoja, Katibu Mkuu inawaniwa na watu wawili, Katibu Mkuu Msaidizi haikupata mtu, Mwekahazina mmoja na wajumbe watano badala ya wanane.

Waliojitokeza katika nafasi ya Urais ni Makamu Mwenyekiti wa TBF, Phares Magesa na John Bandiye, Makamu wa Rais ni Hamis Ally, Katibu Mkuu ni Michael Maluwe ambaye kwa sasa ni katibu mkuu msaidizi na Salehe Zonga wakati Mwekahazina ni Amina Lymaiga.

Wanaogombea ujumbe wa kamisheni ni Manase Zablon, Anjela Bondo, Michael Mwita, Patrick Mapete na Aziz Mwaraka. Mganga alisema kukosekana kwa wagombea wa nafasi hizo hakuzuii uchaguzi kufanyika, bali utaendelea kama ambavyo umepangwa.

Katika hatua nyingine, Katibu msaidizi, Maluwe ameomba wadau mbalimbali kuunga mkono kambi yao ya kujiandaa na maandalizi ya Kombe la Mapinduzi ili kujiandaa vizuri.

Maluwe ameliambia gazeti hili kuwa tayari kikosi cha wachezaji 18 kiliteuliwa wiki hii na kuanza kambi yake ya kujifua kwenye uwanja wa Don Bosco itakayoendelea hadi Januari 7, mwakani.

Alisema kambi inahitaji maji, nauli na vitu vingine muhimu vya michezo. Kwa upande wa usafiri wa kwenda Zanzibar alisema watagharamiwa na wenye mashindano.

Aliwataja wachezaji walioteuliwa hivi karibuni kujifua ni Fadhili Abdallah, Lasser Hill, Arnod Tarimo kutoka Bandari Tanga, Sebastian Marwa ( Pazi), Moses Jackson (Mwanza), Mwalimu Heri (JKT), Lusajo Samwel (Oilers) na Denis Chibula wa Pazi.


CHANZO: HABARI LEO

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.