basketball

UCHAGUZI TBF WAINGIA DOSARI

WAKATI Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), likitangaza kufanyika kwa uchaguzi wake mkuu Desemba 28 mwaka huu mjini Dodoma, makocha wa mchezo huo wameibuka na kuliomba Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kusitisha zoezi hilo kwa manufaa ya mpira wa kikapu nchini.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam jana, Kocha Bahati Mgunda, alisema, ameamua kufikia hatua ya kuiandikia BMT barua kuiomba kuchukua hatua hiyo, baada ya kuwa na ukiukwaji mkubwa wa taratibu/katiba kuelekea zoezi zima la uchaguzi na baada ya kuwasiliana na wadau wengine wa mchezo huo.

“Nimeandika barua ya wazi kwenda BMT kuwaomba wasimamishe zoezi zima la uchaguzi hadi pale kikao cha Bodi ya TBF kitakapokaa na kutoa baraka za kuendesha utaratibu mzima wa uchaguzi huo.

“Pia kikao hicho kitatue au kutoa hitimisho la mgogoro uliopo, ambao umepelekea Katibu Mkuu kusimamishwa na Kamati ya Utendaji,” alisema Mgunda nyota wa zamani wa mchezo huo na kuongeza:

“Kwa mujibu wa Katiba ya TBF, Katibu Mkuu ndiye Mtendaji wa Shirikisho, hivyo anatakiwa kuwasilisha ripoti ya kipindi chote alichokuwa madarakani ikiwamo na mahesabu ya mapato na matumizi yaliyokaguliwa.”

Alisema, ombi jingine ni kuomba wanachama wa msingi wa TBF ambao ni vyama vya mikoa, wafanyiwe uhakiki ikiwa ni pamoja na kuwasilisha ripoti zao kwenye kikao cha Bodi ili kujadiliwa pia.

“Nina wasiwasi kuwa, vyama vingi sio hai na viongozi wake hujitokeza tu wakati wa mikutano mikuu na mikutano ya uchaguzi tu, baada ya hapo hakuna kinachoendelea,” alisema.

Alisema, hadi sasa TBF haijawahi kuitisha mkutano wa bodi wala mkutano mkuu tangu waingie madarakani, ambako masuala yote ya Shirikisho yanafanywa na mtu mmoja hadi wawili tu, jambo ambalo ni kinyume na Katiba ya TBF.

Pia, alielezea kusikitishwa na kitendo cha TBF kushindwa kutoa ushirikiano kwa Kocha Mkuu, Mmarekani Albert Sokaitis na kusababisha kubwaga manyanga, ingawaje uongozi unatoa taarifa potofu kwa jamii.

Naye Kaimu Rais wa Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam, Richard Julius, aliwapongeza makocha kwa uamuzi wao huo na kwamba, wao kama viongozi wa mikoa wako njiani nao kutoa tamko lao kuomba uchaguzi huo usitishwe.


CHANZO: TANZANIA DAIMA

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.