wanawake

PAMOJA NA KUTOLEWA, WAPOKEWA KISHUJAA

TIMU ya soka ya Taifa ya vijana ya wanawake chini ya umri wa miaka 20, Tanzanite juzi ilipata mapokezi makubwa kutoka kwa mashabiki wa timu za taifa waliofika kuipokea kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ikitokea Zambia.

Tanzanite ilikuwa Zambia kucheza mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wa umri huo dhidi ya wenzao wa huko, Shepolopolo ambapo ilitoka sare ya bila kufungana katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Nkoloma Lusaka mwishoni mwa wiki iliyopita.

Hatahivyo, pamoja na kulazimisha sare hiyo, Tanzanite imetupwa nje ya michuano hiyo baada ya kupoteza mechi ya kwanza nyumbani kwa mabao 4-0.

Zambia sasa itacheza hatua inayofuata na Afrika Kusini kuwania kufuzu fainali hizo zilizopangwa kufanyika Papua New Guinea. Msafara wa timu hiyo ukiongozwa na mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya soka ya Wanawake Blassy Kiondo ulifika uwanjani hapo saa nne na nusu usiku na kulakiwa na baadhi ya viongozi wa kamati hiyo na baadhi ya mashabiki wa timu za taifa.

Ilibidi shughuli uwanjani hapo zisimame kwa takriban dakika 15 baada ya wasafiri na wafanyakazi wa uwanja hapo kushangazwa na namna matarumbeta yalivyokuwa yakipigwa na mashabiki hao.

Wachezaji pamoja na viongozi waliosafiri na timu hiyo, nao hawakulaza damu, walijumuika kwa pamoja na kucheza kwa madoido matarumbeta hayo hali iliyofanya baadhi ya wafanyakazi wa uwanjani hapo na wasafiri kutaka kujua kulikuwa na nini. “Kuna nini hapa?... hii ni timu gani? aliuliza msafiri mmoja ambaye aliyeonekana kushangaa kwa sekunde kadhaa kabla hajaendelea na safari yake.

Akizungumza baada ya mapokezi hayo Kiondo alisema wamefarijika kwa namna wadau wa soka walivyojitoa kwa hali na mali kuwaunga mkono. Naye kocha wa timu hiyo, Rogassina Kaijage alisema: “Nimefarijika kwa kweli kuona mapokezi haya, namna hii ndio inatakiwa ili tuwatie moyo vijana wasijione wapweke” .

Akizungumza kwa niaba ya mashabiki hao, Makamu mwenyekiti wakundi hilo Ziota Musisa alisema huo ni mwanzo na kwamba lengo lao ni kuziunga mkono timu zote za taifa.

“Hatuangalii timu ya wanawake wala ya wanaume, kundi letu lengo ni kuziunga mkono timu zetu za taifa, nadhani hata kwenye mechi yenu ya kwanza mliyocheza hapa (Dar es Salaam) mliona kwamba mlifungwa lakini tulipiga matarumbeta mwanzo mwisho,” alisema.

“Tumefarijika sana kusikia mmetoka sare ugenini, wale wenzetu walionekana ni wakubwa kutuzidi lakini tunashukuru kwa matokeo mliyopata, yametupa faraja sana,” alisema

Chanzo: Habari leo

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.