Fabian Joseph avunja rekodi Ngorongoro
Cosmas Mlekani, Karatu
MWANARIADHA wa Kimataifa wa Tanzania, Fabian Joseph (27), amevunja rekodi ya mbio za nusu marathoni za Ngorongoro kwa kutumia dakika 1:03.47.
Joseph, ambaye mwaka jana aliibuka wa kwanza pia, alivunja rekodi hiyo kwa karibu dakika moja, baada ya jana kutimua mbio kwa saa 1:04.
Mshindi wa pili wa mbio hizo zilizoandaliwa na Zara Charity na kudhaminiwa na Kampuni ya simu za mkononi ya Tigo zikiwa na lengo la kupiga vita malaria, alikuwa ni Martine Sulle aliyetumia saa 1;04.26 wakati watatu ni Stephano Huche baada ya kutumia saa 1:04.30.
Kwa upande wa wanawake, wanariadha wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), walitamba baada ya kushika nafasi zote tatu za kwanza wakiongozwa na Jacqueline Juma aliyetumia saa 1:16:01.24, huku akifuatiwa na mwanariadha mkongwe Restituta Joseph aliyetumia saa 1:18.21.83.
Mshindi wa nne katika mbio hizo zilizokuwa na msisimko mkubwa ambazo zilianzia katika lango la kuingilia na kutokea katika hifadhi ya Ngorongoro na kumalizikia mjini Karatu ni Siata Romanus aliyetumia saa 1:20:30.91.
Mbio hizo zilianzishwa na kufungwa na mkuu wa wilaya ya Ngorongoro Elius Wawa Lawi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo.
Hata hivyo, bingwa wa mbio za marathoni wa Michezo ya Jumuiya ya Madola 2006, Samson Ramadhani alijikuta akichemsha baada ya kumaliza katika nafasi ya 18 akimwambia mwandishi wa habari hizi kuwa, amefanya vibaya kwa kuwa hana mazoezi ya kutosha.
Naye Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya riadha ya Tanzania, Zacharia Gwandu alisema baada ya mbio hizo kuwa, Fabian ambaye katika Michezo ya Olimpiki atakimbia mbio za marathoni, alikimbia vizuri jana na ana matumaini ya kufanya vizuri kimataifa pia.
Ramadhani, Fabian na Zakia Mrisho, ambaye alikimbia kilometa tano baada ya kutakiwa kufanya hivyo na Gwandu, wako katika timu ya taifa iliyopo kambini Kibaha kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki itakayofanyika London baadae mwaka huu.
Jacqueline akimaliza baada ya wa kwanza kwa upande wa wanawake alisema kuwa mbio zilikuwa nzuri na ngumu na aliwapongeza waandaaji.
0 comments:
Post a Comment