Mchangani

ABAJALO WATAMBA LIGI YA MABINGWA

TIMU ya soka ya Abajalo FC imeiadhibu Navy FC zote za Mkoa wa Dar es Salaam kwa mabao 4-1 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa wa Mikoa, Kituo cha Mkoa wa Morogoro.

Navy FC ni Mabingwa wa Mkoa huo yenye maskani katika Wilaya ya Temeke, wakati vijana wa Abajalo FC washindi wa pili wa mkoa na maskani yao ni Sinza kwa Remmy wilayani Kinondoni.

Katika mchezo huo wa pili uliofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri hapa, Abajalo iliandika bao la kwanza dakika ya nane lililofungwa na Sultan Kaskas kwa shuti kali baada ya kuipenya ngome ya Navy FC.

Bao la pili lilipatikana dakika ya 17 lililofungwa na Suleiman Ibrahimu kwa shuti kali lililomshinda kipa wa Navy FC, Talib Jecha na mpira kujaa wavuni. Ni baada ya kumtoka beki wa Navy, Muharam Juma.

Mvua ya mabao iliendelezwa na vijana wa Abajalo baada ya Waziri Omary kufunga bao la tatu katika dakika ya 20 kwa njia ya penalti iliyotolewa na mwamuzi Seleman Kinugani wa Morogoro baada ya beki wa Navy FC, Muharami Juma kumfanyia madhambi Kaskas kwenye eneo la hatari.

Karamu ya mabao ya Abajalo ilikamilishwa katika dakika ya 36 kwa bao la nne lililofungwa na mshambuliaji wake, Kaskas aliyewatoka mabeki wa Navy FC na kupachika bao hilo.

Navy ilipata bao la kufutia machozi dakika ya 78 lililofungwa na Alex Kheri baada ya kupokea pasi kutoka kwa Hafidh Abdallah iliyomfikia mfungaji na kupiga shuti la karibu lililomshinda kipa wa Abajalo, Amani Simba na kufanya mchezo huo kumalizika kwa Abajalo kushinda kwa bao 4-1 Katika mchezo wa kwanza uliofanyika juzi, vijana wa Kariakoo FC kutoka Mkoa wa Lindi walitoka sare ya kufungana bao 1-1 na Bulyanhulu FC ya Shinyanga.

Vijana wa Kariakoo, FC walijipatia bao la kuongoza katika dakika ya 36 lililofungwa na Sande Mussa kwa kushuti kali lililomshinda kipa wa Bulyanhulu FC, Zakharia Samwel.

Bao hilo lilitokana na kazi nzuri iliyofanywa na mshambuliaji wa pembeji wa kulia wa Kariakoo FC, Ramadhan Wasso kutoa krosi iliyounganishwa na mfungaji.

Kipindi cha pili, Bulyanhulu FC walimiliki safu ya kiungo na ushambuliaji na kupata bao la kusawazisha dakika ya 78, lililofungwa na Fraiton Michael kwa shuti kali lililomshinda kipa wa Kariakoo FC, Adallah Saidi.



chanzo: habarileo

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.