wachezaji

Cannavaro: utajir wake ni Tsh mil 80

copied from mwanaspoti

BEKI wa kati wa Yanga na Taifa Stars, Nadir Haroub 'Cannavaro' anamiliki mali zinazokadiriwa kuwa na thamani ya sh. milioni 80 na anapenda kukutana na timu pinzani ambayo anayocheza Haruna Moshi 'Boban'. Lakini mchezaji huyo ambaye pia ni nahodha msaidizi wa Zanzibar Heroes, anasema kama angekuwa anacheza soka Unguja angeshakuwa askari.
Mchezaji huyo aliiambia Mwanaspoti jijini Dar es Salaam wiki hii kuwa malengo yake ni kucheza soka popote pale penye amani, masilahi yatakayobadili maisha yake na waliomzunguka.
Nimepiga hatua sana tangu nijiunge na Yanga 2006 nikitokea Tembo FC ya Zanzibar, soka ya huku ni ya ushindani sana na imenisaidia kufikia kiwango cha juu na kujulikana, alisema Nadir ambaye amezaliwa Michenzani, Zanzibar. Soka la Bara lina ushindani sana na hasa katika Simba na Yanga ambako kila mchezaji ndoto yake ni kucheza kwa mafanikio, nafurahi, kila kitu nilichonacho kimetokana na juhudi zangu ndani ya uwanja na kujua nini ninachotakiwa kufanya katika maisha haya.

MALI ZAKE
Katika miaka mitano niliyocheza Yanga nimefanya mambo makubwa sana maishani mwangu ya nje ya uwanja zaidi ya kujuana na watu wengi. Nimeweza kujenga, kumiliki viwanja, magari zaidi ya moja, kuendesha maisha yangu vizuri na familia yangu.
Nimeepukana na maisha duni na ya utegemezi. Siwezi kusema kwamba nimeshakuwa tajiri lakini nina rasilimali zangu ambazo angalau mpaka sasa naweza kumuonyesha mtu kwamba haya ndiyo mafanikio yangu. Siwezi kukutajia kila aina ya kitu cha thamani nilichonacho lakini vyote thamani yake haipungui sh. milioni 80 , kuna nyumba kubwa sana yenye kila kitu ndani naendelea kujenga maeneo ya Mwera pale Zanzibar, ni ghali sana mpaka sasa imenigharimu sh. milioni 41. Nataka ndani ya miezi michache ijayo iwe imeshakamilika na itanigharimu kama sh. milioni 55 ikimalizika kabisa kila kitu, nimejinyima vitu vingi ili kuhakikisha kwamba natekeleza matakwa yangu. Haya ni maisha huwezi kujua nini kitatokea kesho, kinachowezekana leo ni kufanya wakati huo huo.
Nikimaliza kujenga nyumba za Zanzibar nitatulia kidogo nianze nyingine tena Dar es Salaam, pamoja na kuwekeza kwenye miradi mingi zaidi ambayo ni siri binafsi siwezi kusema hadharani.

MAISHA YA SOKA
Nimefurahi kwamba juhudi zangu zimenifanya nionekane na kupewa nafasi kuanzia Yanga mpaka timu za Taifa, sijafika kikomo, nitacheza zaidi ili kuwahamasisha hata mawakala wa nje ya nchi, huwezi kujua nani anakufuatilia. Naweza kupata nafasi kama ya Mrisho Ngassa alivyokwenda West Ham.
Nina kama miaka saba ijayo kucheza soka, baada ya hapo nadhani itakuwa imetosha nitawaachia chipukizi waendelee, na biashara zangu nadhani zitakuwa katika hali nzuri zaidi, itakuwa ni wakati muafaka wa kusimamia miradi yangu na kuendesha familia yangu na kubaki kama shabiki wa soka tu.

NDANI YA YANGA
Mimi naipenda Yanga kwa vile ndicho kituo changu cha kazi kwa sasa, siwezi kuacha kuipenda Yanga wakati ndiyo ofisi yangu na timu inayoniweka mjini na kunipa fedha ya kuendeshea maisha.
Niko kikazi zaidi. Nimepata heshima kubwa sana tangu nijiunge nayo lakini nimepata pia adhabu ya kadi nyekundu mara mbili katika mechi dhidi ya Simba na nyingine ya JKT, ni vitu ambavyo siwezi kusahau.

SIMBA NA YANGA
Inapofika kwenye mechi hizo nakuwa kwenye wakati mgumu sana, inabidi kutumia akili za ziada na kuepuka kufanya makosa ndani ya uwanja. Halafu maandalizi yake huwa yanakuwa ya ajabu sana, mchezaji unaonana na watu wa ajabu ajabu sana kila kukicha, lakini baada ya mchezo huoni hata mmoja.
Huwa nashangaa sana, kama timu zote zingekuwa zinatumia nguvu kwenye mechi za nje kama ilivyo Simba na Yanga tungekuwa mbali sana kwa sababu tuna mashabiki wengi, tena wenye fedha zao, anasema mchezaji huyo ambaye wakala wake ni Hellen Masanja.

BOBAN
Haruna Moshi Boban ni rafiki yangu sana na huwa napenda kucheza na timu yoyote pinzani anayochezea yeye ili nikabiliane naye, napenda sana kucheza naye na yeye huwa anajua, ndiyo maana wakati mwingine kazi inakuwa pevu na mara zote lazima litokee tukio la ajabu. Katika mechi mbili nilizomkaba amekuwa anatumia nguvu nyingi sana na pengine kupandwa na hasira, ndiyo maana anaonyeshwa kadi nyekundu.
Nimecheza naye mechi mbili moja ya Ligi na nyingine ya Kombe la Tusker, zote kapewa kadi nyekundu.

MAXIMO
Marcio Maximo ndiye kocha ambaye siwezi kumsahau kwenye maisha yangu kwa sababu kanipa kujiamini na amenichezesha mechi ya kwanza ngumu dhidi ya Burkina Fasso ugenini tukashinda bao 1-0 , siwezi kusahau, amenijenga sana, anasema mchezaji huyo na kuongeza kuwa ana miaka 26 ingawa kumbukumbu za Fifa na Caf zinaonyesha ana miaka 29.

TAIFA STARS
Kikosi cha Stars sasa kiko imara na lengo langu ni kuweka ukuta imara kuhakikisha kwamba tunashinda mechi dhidi ya Afrika ya Kati. Tukishinda hiyo itasaidia sana, tutakuwa na nafasi, sare haitatusaidia. Nataka tufuzu niweke historia mpya kwa sababu klabu yangu ya Yanga haikuwa na maandalizi mazuri ikashindwa kusonga mbele katika Kombe la Shirikisho.

LIGI KUU
Ligi ina ushindani tofauti na Zanzibar, lakini imefika mahali na klabu nyingine zidhaminiwe ziwe imara zaidi siyo kila siku Simba na Yanga tu. Halafu klabu ziongezwe zifike angalau 20 , Tanzania ni kubwa sana, namna hiyo ndiyo tunapata bingwa imara zaidi.

MIGOGORO
Simba na Yanga ziache migogoro ya wanachama na viongozi ambayo haina maana. Wajipange vizuri na kufanya maandalizi kwa kuangalia mechi za kimataifa zaidi, wasibaki kungangania ligi ya ndani kila siku. Hizi timu kwa hadhi yake si za kuishia hatua ya mtoano au ya kwanza kimataifa, tufikirie tunakosea wapi na tuwe makini, tusichukulie mambo kirahisi.

Maelezo binafsi
Jina kamili: Nadir Haroub Ali
Kuzaliwa: 10 Februari 1982 (29)
Mahali: Michenzani, Zanzibar
Urefu: futi 5.12
Nafasi: Beki wa kati
Klabu: Yanga
Klabu za nyuma: Tembo FC 2002-2005
Timu za Taifa: Zanzibar Heroes, Taifa Stars.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.