VPL

Tegete amlilia Swita

KOCHA mkuu wa timu ya Toto African, John Tegete amesema hajutii timu yake kupata suluhu na Polisi Tanzania ila kadi nyekundu aliyopewa mchezaji wake Emmanuel Swita ndio imemchanganya zaidi kutokana na kutaka kumtumia mchezaji huyo katika mechi dhidi ya Yanga.

Katika mchezo wa juzi dhidi ya Polisi Dodoma timu hizo ziligawana pointi baada ya kutoka 0-0, lakini Toto walipata pigo zaidi pale mwamuzi wa mchezo huo Thomas Mkombozi kutoka Kilimanjaro alipomuonyesha kadi nyekundu Emmanuel Swita baada ya kumchezea vibaya Juma Semsue.

Akizungumza na gazeti hii mara baada ya kumalizika kwa pambano hilo Tegete alisema yeye hajutii kupata pointi moja katika mechi hiyo, lakini kadi nyekundu aliyopewa mchezaji huyo ndiyo imemkosesha raha.

Tegete alisema alitaka kumtumia mchezaji huyo katika mechi yao dhidi ya Yanga kwani anaamini mechi hiyo itakuwa ngumu sana kutokana na wao kutotaka kupoteza pointi kwa ndugu zao hao.

“Safari hii Yanga wasitegemee mteremko kabisa maana tumejiandaa vya kutosha kwa kweli ila kadi nyekundu ya Swita imenichanganya sana, lakini nafasi yake itazibwa tu kwa kuwa nina kikosi imara,” alisema Tegete kwa kujiamini.

Akizungumzia mechi hiyo kocha huyo alisema mchezo huo uliharibiwa na waamuzi kutokana na kuikamia timu yake ambapo amesema alimsikia mwamuzi wa pembeni akimwambia refa awape kadi nyingi wachezaji wake.

“Kwa kweli hawa waamuzi ninawashangaa sana maana nilimsikia mwenyewe huyu mwamuzi wa kulia akimwamuru refa kuwapa kadi nyingi wachezaji wangu hata hivyo kadi nyekundu aliyopewa Swita hakustahili kwa kuwa rafu yenyewe haikuwa kubwa kiasi kile,” alisema Tegete.

Hata hivyo katika mchezo huo mwamuzi wa kati Thomas Mkombozi alionekana kushindwa kumudu mchezo huo huku wakishindwa kuwa na mawasiliano mazuri kati yake na wasaidizi wake wa pembeni hatua iliyofanya mashabiki kuanza kuwazomea.



mwananchi.co.tz

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.