simba

Kiongozi Simba kifungoni maisha


OLIVER ALBERT

KASHFA ya jaribio la upangaji wa matokeo ya mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyoibuka kabla ya kufanyika pambano la watani wa jadi, Simba na Yanga, mwaka jana, sasa inashughulikiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Kiongozi wa Simba aliyehusika na kashfa hiyo iwapo itathibitika alihusika na hilo atafungiwa maisha kwa mujibu wa kanuni za soka.

Takukuru iliithibitishia Mwanaspoti kuwa uchunguzi wa suala hilo unaendelea baada ya kuripotiwa kutokea kabla ya timu hizo kupambana Oktoba 29, mwaka jana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo wa mzunguko wa kwanza, Simba ililala kwa bao 1-0 lililofungwa na Mzambia Davies Mwape.

Habari za kuaminika zilizolifikia Mwanaspoti zinaeleza kuwa Takukuru iliwahoji watu mbalimbali akiwemo kiongozi mmoja wa ngazi za juu wa Simba (jina tunalo) na wachezaji wa Yanga, wiki iliyopita.

Msemaji wa Takukuru, Doreen Kapwani, alikiri kuwa suala hilo lilikuwa mezani kwao ingawa hakutaka kuingia kwa undani kuhusiana na uchunguzi wao.

�Hilo suala limefika mikononi mwetu na linafanyiwa kazi, liko chini ya upelelezi na ukikamilika tutatoa tamko na kujua hatua gani zitachukuliwa.

Mwanaspoti, hata hivyo, linafahamu upelelezi wa suala hilo unamhusisha kiongozi huyo wa ngazi ya juu wa Simba.

Kiongozi huyo wa Simba inadaiwa alimpigia simu mshambuliaji wa Yanga, Pius Kisambale kabla ya mchezo huo.
Kisambale alipigiwa simu wakati timu yake ilipokuwa imeweka kambi katika hoteli ya Double Tree iliyoko Masaki, jijini Dar es Salaam.

Uchunguzi wa kina uliofanywa na Mwanaspoti, unaeleza kuwa kigogo huyo, hata hivyo, inadaiwa alipiga hesabu mbovu kwani wakati anapiga simu ile, Kisambale alikuwa na baadhi ya viongozi wa Yanga (majina tunayo).

Simu ya kiongozi huyo inadaiwa ilizua mshituko miongoni mwa viongozi wa Yanga na Kisambale alilazimika kuongeza sauti ili viongozi wake wasikie wanateta kitu gani na kigogo huyo wa Simba, alisimulia mtu mmoja aliyekuwepo kwenye tukio hilo.

Shuhuda wa tukio hilo anaeleza kwamba mshambuliaji huyo alirekodi maneno ya kiongozi huyo mzito wa Simba, kitendo ambacho pia kilifanywa na viongozi waliokuwa wamemzingira.

Chanzo hicho cha kuaminika kilisema kuwa kigogo huyo wa Simba alimwomba mshambuliaji huyo wa Yanga akipangwa katika mchezo ule acheze chini ya kiwango na kumwahidi 'mzigo' na inasemekana alimwomba aongee na wenzake ili awaeleze juu ya mpango huo mchafu.

Kila kitu kilinaswa na viongozi wa Yanga na walikasirishwa na hatua ile na kushupalia suala hilo lazima lifikishiwe kwenye ngazi zinazohusika kisheria ili mhusika achukuliwe hatua kali za kisheria na kukomesha tabia hiyo.

Kwa kauli moja, viongozi hao waliamua kufikisha suala hilo Takukuru ili kiongozi huyo wa Simba ajibu madhambi yake.

Habari za kuaminika zinaeleza kuwa Takukuru ilimhoji Kisambale na wachezaji wengine wa Yanga, wiki iliyopita katika ofisi yao iliyoko Upanga jijini Dar es Salaam kuhusiana na kashfa hiyo.

�Kisambale amehojiwa na Takukuru na baadhi ya wachezaji wa Yanga na hata kigogo mwenyewe wa Simba naye alikuwa ameitwa kuhojiwa na sijui itakuwaje maana hili jambo limefika pabaya.

�Watu wamechoka na rushwa katika mechi za ligi kwani inadumaza soka la nchi yetu na ndiyo maana wameling�ang�ania suala hili, ngoja tusubiri ukweli utakuwa upi, ila mtuhumiwa wa jambo hili ana kazi kwani ushahidi wa simu ndio utamweka matatani zaidi,� kilidokeza chanzo hicho ambacho kiko karibu na uchunguzi wa suala hilo.

Kisambale alipoulizwa juu ya suala hilo, aligoma katakata kuliongelea kwanza na baadaye kusema hafahamu chochote kuhusu suala hilo.

Mwanaspoti ilimtafuta Katibu Mkuu wa Yanga, Celestine Mwesigwa ambaye aliruka na kudai hawezi kulizungumzia.

�Ishu gani? Siwezi kuzungumzia kama mnataka kamuulizeni huyo kiongozi wa Simba mwenyewe, haya mambo yako katika vyombo vya sheria siwezi kukurupuka kusema chochote,� aliongeza Mwesigwa.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa upelelezi umehusisha mawasiliano mbalimbali ya simu kati ya wachezaji wa Yanga na kigogo huyo wa Simba.

Habari zaidi zinaeleza kuwa uchunguzi wa sakata hilo umekwenda mbali zaidi kiasi cha kunasa mawasiliano ya baadhi ya waandishi wa habari za michezo (majina yao tunayo) kutokana na namba zao za simu kuonekana zilitumika katika mawasiliano kati yao, kigogo huyo wa Simba na wachezaji wa Yanga.

Mwanaspoti pia limedokezwa pia na vyanzo vya kuaminika kuwa suala hilo si pekee linalochunguzwa na Takukuru bali pia kuna jaribio la kutaka kumhonga kipa wa zamani wa Mtibwa, Shabaan Kado nalo pia linafanyiwa uchunguzi.

Tukio hilo lilitokea msimu wa 2010/2011 wakati mshambuliaji wa Simba, Ulimboka Mwakingwe kwa wakati huo hakuwa na timu, alipokamatwa huko Turiani na walinzi wa kiwanda cha sukari cha Mtibwa.

Mwakingwe inadaiwa alikwenda huko baada ya kutumwa na kiongozi wa Simba ili amkabidhi 'mzigo wake' kabla ya mechi ili aachie mabao wakati wa mechi ya Simba na Mtibwa katika msimu huo.

Kado, ambaye kwa sasa anaidakia Yanga, inasemekana naye amehojiwa na Takukuru kuhusiana na suala hilo.
Alipoulizwa kuhusiana na mahojiano hayo, Kado alikataa kuzungumzia chochote na Mwanaspoti.

Matokeo ya uchunguzi wa suala hilo yanatarajiwa kutikisa medani ya soka la Tanzania, ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikitawaliwa na minong'ono ya upangaji matokeo na hasa mechi za watani wa jadi.

Ikiwa kigogo huyo wa Simba atakutwa na hatia, atajikuta matatani kwenye medani ya soka kwa mujibu wa Kanuni za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Sehemu ya sita inayozungumzia masuala ya Nidhamu ya Fifa inaainisha hukumu ya makosa yanayotokana na watoa rushwa kwenye soka.

Vifungu (a), (b) na (c) vya Kanuni hizo za Fifa zinaeleza kuwa mtuhumiwa anaweza kuadhibiwa kwa kufungiwa maisha, faini ya Sh17 milioni, au kutoruhusiwa kabisa kuingia katikia kiwanja chochote cha soka akibainika kufanya makosa hayo.

Pia Fifa inaweza kuandaa utaratibu wa kufilisi mali za mtuhumiwa na mali zake kutumika kuendeleza soka ikiwa atahusishwa na masuala ya kutoa rushwa kwa waamuzi.

Kwa miaka mingi wachezaji wa Simba na Yanga wamekuwa wakiadhibiwa kila baada ya mechi zinazokutanisha timu hizo mbili na hasa pale timu moja inapopoteza mchezo.

Tukio hilo limetokea siku chache baada ya kocha wa Miembeni, Salum Bausi, kujiuzulu baada ya kukasirishwa na kitendo cha wachezaji wake kuiachia Simba na wakafungwa 4-3 kwenye Kombe la Mapinduzi kimizengwe.

Tukio jingine la rushwa kwenye soka lililowahi kutikisa soka la Tanzania lilikuwa mwaka 1984 wakati viongozi wawili wa Yanga, Julius Rutainulwa na Issa Makongoro walipofungiwa maisha na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) baada ya kujaribu kuwahonga waamuzi wa Ethiopia wakati wa mechi ya Klabu Bingwa Afrika kati ya timu yao na Gor Mahia ya Kenya.

Ni mara chache shirikisho linalosimamia mchezo huo nchini limejitokeza kupambana na upangaji matokeo kama mwaka 1987 wakati Simba ilipofungana 5-5 na Tukuyu Stars na timu nyingine zilikumbwa na kashfa hiyo na zilipigwa faini tu ingawa kosa hilo hukumu yake ni kushushwa daraja.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mwaka 2008 liliwaadhibu waamuzi Othmani Kazi, Omari Miyala na Omari Mfaume baada ya kubainika kupokea rushwa ya Sh200,000 ili kuipendelea Majimaji ilipocheza na Mtibwa kwenye mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Pamoja na ukweli kuwa vyombo vinavyohusika huwa halivipi uzito unaostahili suala la rushwa katika soka kwa Tanzania lakini masuala haya ni ajenda kubwa katika medani ya soka la kimataifa.

Kuliwahi kutokea mtikisiko mkubwa katika medani ya soka la Ufaransa mwaka 1994 baada ya Rais wa Olympic Marseille, Bernard Tapie kutuhumiwa kuhonga timu pinzani na matokeo yake timu yake ikashushwa daraja kutoka Ligi Kuu.

Ilivuliwa ubingwa wa msimu wa 1992�93 na kupokonywa haki ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, Super Cup na Kombe la Klabu Bingwa la Dunia baada ya kuhusishwa na kashfa ya kununua mechi.

Olympique de Marseille inadaiwa iliwahonga wachezaji wa Valenciennes, Jacques Glassmann, Jorge Burruchaga na Christophe Robert ili wacheze chini ya kiwango.

Kama ilivyokuwa kwa wachezaji wa Simba, inadaiwa walipigiwa simu na mchezaji wa Marseille, Jean-Jacques Eydelie, wakiahidiwa fedha ili wacheze chini ya kiwango na pia wahakikishe hawachezi rafu ili wachezaji wa Marseille wasiumie kwani walikuwa wanakabiliwa na mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 1993.

Kufuatia kashfa hiyo ya rushwa, Tapie, ambaye aliwahi kuwa Waziri katika serikali ya Ufaransa, alijikuta akifungwa miaka miwili jela kutokana na makosa hayo.

Tukio jingine ambalo lilitikisa soka la kimataifa ni lile la kashfa ya rushwa na upangaji wa matokeo ya mechi za ligi iliyotokea Italia iliyojulikana kama Calciopoli mwaka 2006.

Kashfa hiyo ilihusisha timu za Ligi Kuu Italia na zile za Daraja la Kwanza baada ya uchunguzi wa polisi.

Timu zilizohusishwa na kashfa ile ni pamoja na Juventus, AC Milan, Fiorentina, Lazio na Reggina baada ya mawasiliano ya simu kati ya viongozi wa timu hizo na waamuzi kunaswa wakati wakipanga mikakati ya kuhongana.

Juventus iliyokuwa bingwa wakati huo ilituhumiwa kutoa rushwa ili kupangiwa waamuzi inaowataka, kwa makosa hayo ilishushwa daraja na pia timu nyingine za Fiorentina na Lazio.

Pia Meneja wa zamani wa Juventus, Luciano Moggi amefunguliwa mashtaka ya makosa ya jinai kwa makosa ya rushwa.

Kashfa za watu kununua mechi zimewahi pia kutokea huko Brazil mwaka 2005 baada ya mwamuzi Edilson Pereira de Carvalho kufungiwa maisha na Paulo Jose Danelon kuondolewa kwenye orodha ya waamuzi wa Paulista kutokana na kupokea rushwa ya makampuni ya kamari ili kupanga matokeo ya mechi.

Huko Uturuki mwaka 2011, polisi wa Uturuki walianzisha uchunguzi mkali kwa mechi 19 za ligi ya nchi hiyo baada ya kutokea habari kulikuwa na upangaji wa matokeo.

Watu wapatao 61 walikamatwa wakiwemo viongozi wa klabu na wachezaji wa timu ya taifa ya Uturuki baada ya kutajwa walikuwa wanafanya biashara ya kuuza na kununua mechi za soka.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.