wachezaji

Enzi za Ngulungu

copied Habari leo

“USWAHIBA wa timu ya Coastal Union ‘ Wagosi wa Kaya’ ya Mkoa wa Tanga na Simba ulianza kuingia dosari kuanzia mwaka 1990 , pale wagosi wa Kaya tulipoweka ngumu kutoa mwanya wa ushindi kwenye mchezo wetu na Simba, tuliwafunga na wakashindwa kujitangazia ubingwa wa Bara kabla ya ligi kumalizika,” hiyo ni kauli ya Idrissa Ngulungu. Ngulungu ni mchezaji wa zamani wa Coastal Union ambaye aliwika na timu hiyo kuanzia mwaka 1984 hadi mwaka 1999 akicheza nafasi mbalimbali uwanjani, ingawa zaidi ilikuwa nafasi ya kiungo. Kiungo huyo anaweka wazi chanzo cha uhasama uliojitokeza baina ya viongozi wa Coastal Union na maswahiba wao wakuu timu ya Simba uliojitokeza msimu wa ligi ya mwaka 1990. “Mwaka 1990 Coastal Union ilikuwa na nafasi nzuri ya kuweza kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara sawa na Simba na Yanga. “Lakini Simba ndiyo walikuwa na nafasi nzuri zaidi ya kutwaa ubingwa huo kabla ya kumalizika kwa ligi, walichohitaji ni kushinda mchezo wao dhidi yetu ili watangazwe mabingwa wakiwa wamebakiza mechi tatu mkononi,” anasema Ngulungu. Lakini anasema Coastal pia walibakiwa na michezo mitatu ukiwemo wa Simba na endapo wangeshinda michezo hiyo huku Simba na Yanga wakipoteza michezo hayo mitatu waliokuwa nayo, Coastal Union ingekuwa na nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa huo. “ Tuliambizana hapa, hakuna uswahiba ni kucheza mpira, tuliweka pembeni mahusiano kati ya viongozi wa Simba na Coastal Union, hatukupenda wajitangazie ubingwa mikononi mwetu, tukacheza kufa kupona na tukaibuka washindi wa bao 1-0. “ Mshambuliaji wetu Juma Mgunda ndiyo aliyefunga bao hilo kwa shuti kali, ambalo lilishinda kipa wa Simba wakatihuo, Makenzie Ramadhani,” anasema Ngulungu. Anasema baada ya kuwafunga katika mchezo huo, uhasama ndipo ulipoanzia, ambapo mashabiki wa Simba na viongozi wao kujenga chuki dhidi ya Coastal Union zilizojionesha moja kwa moja na hali hiyo ilijidhihirisha wakati wa michezo yao iliyofuatia jijini Dar es Salaam. “ Tulipokwenda kucheza na timu ya Sigara pamoja Yanga jijini Dar es Salaam, mashabiki wa Simba walituzomea uwanjani na hata kudiriki kututupia chupa tupu za maji,“ anasema Ngulungu. Anasema mwaka huo, Coastal Union ilifanikiwa kushika nafasi ya pili na kwamba licha ya Simba kufungwa na Yanga kwenye mchezo wake, iliweza kutwaa ubingwa huo wa Bara mara baada ya kuifunga timu ngumu ya African Sport ‘ wanakimanumanu‘ pia ya mkoani Tanga. Hata hivyo anasema Coastal Union katika miaka hiyo ilipata mafanikio makubwa kwanza kabla ya kujiunga nayo, timu hiyo ilifanikiwa kutwaa Kombe la Opareshani Futa Mdeni ( OFUMA) chini ya iliyokuwa FAT na pia kwa mara ya kwanza na ya mwisho ilitwaa ubingwa wa Bara mwaka 1988 , wakati huo akiwa ni miongoni mwa wachezaji wa timu hiyo. Mchezaji huyo anasema kuwa, kabla ya kujiunga na Coast Union ya Tanga, alianzia kuchezea Tumbaku ya Morogoro mwaka 1980 hadi mwaka 1981 na kuachana na timu hiyo baada ya Kampuni ya Tumbaku kupunguza wafanyakazi wakiwemo baadhi ya wachezaji wa soka wa timu hiyo. Anasema mwaka 1982 aliamua kwenda mkoani Tabora na akiwa huko walianzisha timu ya Tindo iliyokuwa ikimilikiwa na Idara ya Ujenzi. Kwa mujibu wa mchezaji huyo, akiwa na Tindo kwa ujumla wao walijitahidi ipande daraja la kwanza, lakini ilikabiliwa na ushindani wa timu zilizokuwa zimeshuka daraja. “ Nikiwa na timu hii ya Tindo kuanzia mwaka 1983 na 1984 , tuliweka mikakati ya kuipandisha daraja la kwanza, lakini ushindani ulikuwa ni mkubwa wa kipindi hicho na mwaka huo timu ya Pamba ya Mwanza ilipanda daraja na mwaka uliofuatia (1985) timu mbili, RTC Kagera na Nyota Nyekundu ya Dar es Salaam nazo zilipanda,” anasema. Anasema mwaka 1984 , alipokuwa na Tindo kwenye kituo cha Tanga pamoja na Coastal Union, ndipo wagosi wa kaya walifanikiwa kupanda daraja la kwanza, ambapo viongozi wa timu hiyo walimsajili kwenye timu yao. “Nilianza rasmi kuichezea Coast Union mwaka 1985 hadi kufikia mwaka 1993 , na baadaye nikahamia timu ya Pan African, niliichezea msimu mmoja wa 1993 ambapo mwaka 1994 nilihamia timu ya Reli ya Morogoro,” anasema Ngulungu. Hata hivyo baada ya timu ya Coastal Union kushuka daraja mwaka 1993 na baadaye kupanda tena mwaka 1995 , viongozi wa timu hiyo waliamua kuwaita tena wachezaji wote walioondoka baada ya kushuka daraja. Aliwataja baadhi ya wachezaji walioitwa na kurejea tena kwenye timu hiyo mbali na y eye ni Razack Yusuph ‘Carecca’, Yassin Napili, Juma Mgunda, Joseph Lazaro na Said Korongo. Ngulungu, alifichua siri ya mafanikio ya soka ya miaka hiyo kwa Mkoa wa Tanga, kuwa ilitokana na viongozi wa Mkoa huo hasa wazawa kujawa na mapenzi ya soka, hivyo walijitolea kuzisaidia klabu zao kwa hali na mali. “Vipaji vingi vya wachezaji vilikuwepo Mkoa wa Tanga, sasa vimetoweka na hiyo imetokana na mabadiliko ya maisha na viongozi wa timu kama African Sports na Coastal Union ambao baadhi yao wapo mbele ya haki, baadhi ya waliopo hawana mapenzi ya dhati na ukichangana ya hali ya uchumi wa kifedha, inakuwa ngumu,” anasema Ngulungu. Hata hivyo anasema, wakati wote akiwa na Coastal Union, kumbukumbu inayoweza kumfanya asiisahau ni pake mwaka 1991 timu hiyo iliposhiriki michuano ya Kombe la Afrika Mashariki na Kati yaliyofanyika kwenye vituo viwili, Tanga na Dar es Salaam. “Sisi wenyeji tulibakia Tanga na moja ya timu iliyopangwa kituo hiki ni Limbe Leaf ya kutoka nchini Malawi, wachezaji wa timu hii walitudharau wakisema kuwa wamepangiwa kucheza na wanafunzi wa shule ya Msingi,” anasema Ngulungu. “Siku ya mchezo, baadhi ya wachezaji wa Limbe Leaf walitushika mikononi wakituonea huruma kwa vile sisi ni wanafunzi na hii ilitokana na maumbile yetu ya mwili kuwa madogo pamoja na vimo, walicheza kwa kutudharau, “ anasema. Hata hivyo katika mchezo huo, walitumia udhaifu huo wa kudharauliwa kuwa wao ni wanafunzi, kucheza kwa bidii na kufanikiwa kutoka sare ya bila kufungana na baadaye Coastal Union kushika nafasi ya kwanza katika kituo hicho na Limbe Leaf kumaliza wa pili. “Coastal Union tulijitoa baadaye kufuatia kutoelewana na waandaaji na wadhamini wa mashindano hayo pale walioamua kuhamishia michezo ya kituo kwenda jijini Dar es Salaam kwa mshindi wa kwanza na wapili,” anasema Ngulungu. Pamoja na kuichezea timu hiyo kwa muda mrefu, watu wa Mkoa wa Tanga bado wanazo kumbukumbu yake pamoja na yeye kwa kuifungia mabao mawili timu hiyo kati ya matatu dhidi ya Yanga mwaka 1991. “ Nimeacha historia ya jina langu Mkoani Tanga, wanaonifahamu hasa wapenzi wa sokahunikumbuka hasa kwa mchezo wetu na Yanga nilipopachika mabao mawili kati ya matatu. “Nilifunga bao la kwanza na la tatu, ulikuwa mchezo mkali , bao la pili lilifungwa na Kingsley Malwilo na mpira unamalizika kwa kuwafunga Yanga bao 3-1 , “ anasema Ngulungu. Kwa mujibu wa mchezaji huyo, kati ya wachezaji ambao waliwahusudu kutokana na uwezo wao ni pamoja na aliyekuwa kiungo wa timu ya Majimaji ya Songea, Octavian Mrope, alikuwa na uwezo wa kumiliki mpira na nguvu nyingi. Ngulungu pia anamtaja mwingine ni kiungo wa zamani Kalfan Ngassa, aliyekuwa na timu ya Pamba, anamtaja kuwa ni mchezaji aliyekuwa na akili nyingi sana akiwa na mpira miguuni sambamba na kasi. Anasema wachezaji wa siku hizi wanakosa ubunifu na kujituma, tofauti na miaka yao ambapo walikuwa ni ubunifu ulioweza kuwasaidia walimu wao katika uchezaji na kwamba bado wanakosa uwezo wa kupiga mashuti ya umbali wa mita 30 hadi 40 sambamba na kushindwa kudumu muda mrefu katika timu zao. Akizungumzia maisha yake baada ya kustaafu kucheza mpira, anasema anajishughulisha na biashara ya kuuza vifaa vya michezo hasa jezi kwa klabu za ngazi za chini zinazoanzishwa na vijana wenyewe ama makundi ya taasisi za michezo. “Nimeamua kufanya biashara hii kutokana na kuwepo kwa hamasa ya vijana kupenda mpira na kuanzisha timu zao, nafuata vifaa hasa jezi Dar es Salaam na kuwauzia vijana wenye kuunda timu zao, ninapata faida inayonisaidia kuendesha maisha yao,” anasema Ngulungu. Mchezaji huyo mzaliwa wa Mkoa wa Morogoro alizaliwa miaka 49 iliyopita, amepata elimu ya msingi katika shule ya Mwembesongo hadi kufikia darasa la saba na ana mke na watoto watano kati yao watatu ni wakike na wawili ni wa kiume.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.