MWENYEKITI wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage amesema atatii maagizo ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) yaliyotolewa hivi karibuni.
Hivi karibuni, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, ilimtambua Rage kuwa Mwenyekiti halali wa Simba na kumtaka kuitisha Mkutano Mkuu kwa mujibu wa taratibu za Simba.
Ilifikia hatua hiyo baada ya kubaini upungufu kadhaa wa kisheria kwenye uamuzi wa Kamati ya Utendaji ya Simba wa Novemba 18, 2013 wa kumsimamisha Rage.
Akizungumza jana kwa simu akiwa jimboni kwake Tabora Mjini, Rage aliipongeza Kamati ya Utendaji pamoja na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kwa kumtambua kuwa Mwenyekiti halali wa Simba.
“Nimepokea barua ya Kamati ya Sheria iliyoandikwa Desemba 30, imenifikia hapa Tabora Desemba 31. Nawashukuru sana kwa kunitambua kuwa Mwenyekiti halali wa Simba,” alisema Rage na kuongeza: “Wamenitaka niitishe Mkutano Mkuu wa Uchaguzi kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti kwa kuzingatia Katiba ya Simba. Sina tatizo, nitatii na kutekeleza maagizo yote ya TFF”.
Rage ambaye ni Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), alisema atafanya hivyo kwa kuwa TFF wametambua ndiye mwenye mamlaka ya kuitisha Mkutano Mkuu kwa mujibu wa Katiba ya Simba na si vinginevyo.
“Nitakutana na Kamati yangu ya Utendaji na kupanga utekelezaji wa maagizo haya ya TFF, kwa sababu wametambua kuwa kikatiba, Mwenyekiti ndiye mwenye mamlaka ya kuitisha Mkutano Mkuu,” alisema.
Kwa mujibu wa Katiba ya Simba, uchaguzi utaitishwa baada ya notisi ya siku 90 yaani miezi mitatu, hivyo hadi kufikia mwishoni mwa Machi mwaka huu, Simba watatakiwa kupata Makamu Mwenyekiti. Nafasi hiyo iko wazi baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa akiishikilia Geoffrey Nyange ‘Kaburu’.
Hata hivyo, tangu uamuzi wa Kamati ya Utendaji ya Simba kutangaza kumsimamisha Mwenyekiti wao, kumekuwapo na sintofahamu Msimbazi kwa baadhi ya wanachama wakitaka Rage ajiuzulu, jambo analolipinga akisema Katiba ilikiukwa.
Hivi karibuni, alisema kuwa suluhu pekee ya kuinusuru Simba na mgogoro huo wa uongozi ni kuitisha mapema Uchaguzi Mkuu kabla ya kumalizika kwa muda wao, Mei mwaka huu.
Wenzake wamepinga hilo. Katika taarifa yake, Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji, ilisema upungufu uliofanywa na Kamati ya Utendaji ni pamoja na ukiukwaji wa Ibara ya 33 ya Katiba ya Simba juu ya uitishaji wa mkutano, ajenda ya kumsimamisha Mwenyekiti kuwasilishwa kwenye kikao kwa utaratibu wa mengineyo.
Aidha, ilisema imegundua ukiukwaji wa maadili katika suala hilo, hivyo, litapelekwa katika kamati husika. Ukiukwaji huo ni kwa Kamati ya Utendaji kufanya mapinduzi haramu ambayo kwa mujibu wa TFF, adhabu yake ya chini ni kifungo cha miaka 10 cha kutojihusisha na soka na maisha kikiwa ni cha juu.
CHANZO: HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment