basketball

AZAM MEDIA WAIDHAMINKI BASKETBALL DAR


KAMPUNI ya Azam Media imejitokeza kudhamini mashindano ya Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi mwishoni mwa wiki hii, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Mpira wa Kikapu Dar es Salaam (BD), Jimmy David alisema udhamini wa Azam Tv na Azam Cola ni mwanzo mzuri wa kurudisha mchezo huo mahali pake kwani ulikuwa umekufa.
“BD imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha mchezo wa kikapu unarudi mahali pake, kutokana na ukweli kwamba mchezo huu una wapenzi wengi ambao wamekuwa wakinyimwa fursa ya kuufurahia mchezo waupendao, kama ilivyofanya Azam na wadau wengine wajitokeze pia,” alisema David.
Alisema Azam imekubali kuonesha michezo hiyo ya ligi itakayooneshwa moja kwa moja kupitia runinga hiyo kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, ili kurudisha thamani ya mchezo huo.
David amewahimiza wadau wengine zikiwamo kampuni kujitokeza na kuwaunga mkono michuano hiyo kwa maendeleo ya mchezo huo.
Naye Mratibu wa mashindano hayo, Mwenze Kabinda alisema siku ya ufunguzi keshokutwa, kutakuwa na mchezo utakaowashirikisha mastaa waliowahi kucheza miaka ya nyuma, ukienda sambamba na burudani ya muziki.
Alisema katika mchezo huo hakutakuwa na kiingilio chochote ili kuwapa nafasi mashabiki kujitokeza kwa wingi kushuhudia timu zikichuana kwa ushindani.
Naye Mkuu wa Idara ya Ubunifu ya Azam Tv, Geoffrey Lea alisema lengo la kampuni hiyo ni kuhakikisha mchezo huo unachezwa. “Hii ni aina ya ushirikiano baina yetu na Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam, 

tumeunga mkono ili kuona na taasisi nyingine zinajitokeza kuwasaidia kutimiza malengo yao,” alisema Lea.
Timu zitakazoshiriki ni JKT, ACB, Mgulani, Kurasini Heat, Magereza, Savio, Vijana, Jogoo, Chui, Don Bosco Osterbay, Pazi na Oilers.

About Unknown

0 comments:

Powered by Blogger.