BENKI ya NMB imetoa Sh milioni 19.4 kwa ajili ya kudhamini mashindano
ya gofu ya taifa ya kama Nyerere Master mwishoni mwa wiki hii kwenye
viwanja vya Gymkhana Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Gofu Tanzania
Joseph Tango alisema zaidi ya wachezaji 100 kutoka mikoa mbalimbali ya
Tanzania Bara wanatarajia kushiriki mashindano hayo ambayo pia
yatashirikisha wachezaji wa rika tofauti tofauti.
Tango alisema katika mashindano ya mwaka huu watatumia matundu 30
siku ya kwanza wakitumia mashimo 18 na siku ya pili na ya mwisho
watatumia tena mashimo 18 na kukamilisha idadi hiyo ambayo kitaalamu
inakidhi haja kutokana na wingi wa klabu zinazo shiriki.
“Tunawashukuru NMB kwa kuendelea kudhamini mashindano yetu kwa mwaka
wa tatu sasa na kitu cha kufurahisha ni kwamba zawadi kwa mwaka huu
zimeongezeka katika kila umri na mashindano haya yana faida kubwa kwa
taifa kubwa, ikiwa ni kusaidia kupata wachezaji wa timu za taifa,”
alisema Tango.
Kwa upande wake Filbert Mponzi kutoka NMB ambaye ni Mkuu wa Huduma za
kibenki kwa kampuni kubwa, alisema dhamira yao ya kuendelea kudhamini
mashindano hayo ni kutokana na heshima na kumbukumbu ya kifo cha Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Alisema kitu kingine kinachowasukuma kuendelea kudhamini mashindano
hayo ya gofu kwa mwaka wa tatu mfululizo ni lengo lao la kuendeleza
michezo na kulitangaza taifa katika anga za kimataifa.
“Tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi Jumamosi na Jumapili kuja
kushuhudia mashindano haya ambayo kiukweli yana ushindani mkubwa tofauti
na watu wanavyofikiria,” alisema Mponzi.
CHANZO: HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment