riadha

RT kuchagua timu ya vijana Februari 21

MASHINDANO ya kusaka timu ya taifa ya riadha itakayoshiriki michuano Afrika Mashariki na Kati kwa vijana wenye umri chini ya miaka 19 itakayofanyika baadae nchini, yatapigwa Februari 21, imeelezwa.

Kaimu Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania (RT), Ombeni Zavalla alisema kuwa, mashindano hayo ya mchujo yatafanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa mashindano ya Afrika Mashariki yatafanyika pia kwenye uwanja huo huo kuanzia Aprili 22 na 23 mwaka huu.

Alisema kuwa RT inaendelea na maandalizi ya mashindano yote mawili, ambapo tayari imetuma mialiko kwa timu za nchini ambazo zitashiriki mashindano hayo ya mchujo.

Zavalla alisema pia wameshatuma barua za mialiko kwa timu shiriki, ambazo ni Kenya, Uganda, Ethiopia, Sudan na Sudan Kusini, Eritrea, Rwanda na Burundi.

Akizungumzia mashindano ya mchujo, Zavalla alizitaka klabu zitakazoleta wachezaji kuzingatia umri na kuendelea kuwaandaa wachezaji wao kwa ajili ya mashindano hayo.

Aidha, kambi ya riadha kwa ajili ya maandalizi ya kushiriki Michezo ya Olimpiki inatarajia kuanza leo West Kilimanjaro. Zavalla alithibitisha kuwa baadhi ya wanariadha jana walianza kuwasili mjini Moshi tayari kwa kambi hiyo chini ya makocha Francis John na Zacharie Balie.

CHANZO: HABARI LEO

About dada

0 comments:

Powered by Blogger.