vilabu

MAYANGA AMTAKA CASILLAS AZIBE PENGO LA KAKOLANYA

KOCHA wa Tanzania Prisons Salum Mayanga, amesema anajipanga kuhakikisha anaibomoa Mtibwa Sugar kwa kumsajili kipa Hussein Sharifu, ‘Casillas’ kwa ajili ya kuziba nafasi ya Beno Kakolanya, aliyejiunga na Yanga.

Casillas amekosa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza cha kocha Mecky Maxime tangu aliporejea timu hiyo akitokea Simba na kumuacha Said Mohamed akitamba kwenye nafasi hiyo karibu msimu mzima wa ligi iliyomalizika.

Akizungumza na gazeti hili Mayanga, aliyewahi kuwa kocha wa Mtibwa siku za nyuma, alisema anafahamu uwezo wa Casillas na ndiyo maana anataka kumchukua ili wakafanye naye kazi akiamini ataziba vizuri nafasi hiyo.

“Najua siwezi kupata ushindani kwa sababu nina mahusiano mazuri na uongozi wa Mtibwa Sugar, naamini hawawezi kuninyima kipa huyo ambaye kwangu naamini atanisaidia kwenye msimu ujao,” alisema Mayanga.

Alisema pamoja na kukaa benchi lakini kwa kipindi atakachokuwa naye mazoezini atahakikisha anamnoa na kurudisha makali yake yaliyomfanya asajiliwe na Simba na kuitwa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.

Prisons ilimaliza nafasi ya nne msimu uliopita huku kazi kibwa ikifanywa na kipa wake Kakolanya, ambaye baada ya ligi kumalizika, alinyakuliwa na mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga ili kuongeza ushindani kwa makipa waliopo Ally Mustapha ‘Barthez’ na Deogratius Munishi ‘Dida’.

Chanzo: Habari leo

About Unknown

0 comments:

Powered by Blogger.