KAMPUNI ya Utoaji Huduma za Simu za Mikononi ya Vodacom huenda ikajitoa katika udhamini wa Ligi Kuu ya Bara mara baada ya kukamilika kwa mkataba wake wa miaka mitano ya udhamini wa ligi hiyo.
Hali hiyo inakuja kutokana na mambo mbalimbali ikiwemo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutoridhika na mchakato wa Vodacom kuiruhusu Yanga kutumia nembo yenye rangi nyeusi badala ya nyekundu inayotumiwa na kampuni hiyo katika jezi zake.
Rais wa TFF, Leodegar Tenga alisema baada ya Vodacom kuingia mkataba kienyeji na Yanga wa kubadili rangi ya nembo, wao kama shirikisho wameiandikia kampuni hiyo ya simu na kuieleza klabu yoyote itakayobadili rangi ya nembo, hawatowajibika kwa lolote.
“Tumewaambia Vodacom, sasa klabu yoyote ikitaka kubadili rangi za nembo ya Vodacom wafanye watakavyo kwani walivyofanya na Yanga (kuingia mkataba kienyeji) si jambo la kiungwana,” alisema Tenga.
Hata hivyo katika hali ya kawaida, si jambo rahisi kwa Vodacom kukubali nembo yake ibadilishwe rangi na klabu zitakazoshiriki ligi hiyo kwani nafasi yake kibiashara inaweza kuyumba.
Mambo yote ya mkataba pia yatategemea na faida iliyopata Vodacom kutokana na ushiriki wake katika udhamini wa ligi hiyo kubwa kwa ngazi ya klabu hapa nchini. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa mwezi huu na Tume ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Vodacom ndiyo kampuni inayoongoza kwa kuwa na wateja wengi wanaotumia simu za mikononi ikifuatiwa na kampuni nyingine.
KAMATI YA LIGI KUTAMBULIKA OCTOBER.
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), liko katika hatua za mwisho kukamilisha mchakato wa uanzishaji kamati huru ya kusimamia Ligi Kuu na ile ya Daraja la Kwanza.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Rais wa TFF, Leodegar Tenga, alisema hadi sasa wamefikia mahali pazuri ambapo kamati hiyo itawekwa hadharani Oktoba mwaka huu. Tenga alisema uamuzi huo ni katika kuipunguzia mzigo Kamati ya Mashindano na kuongeza ufanisi katika ligi hizo mbili, ambazo ndizo kubwa hapa nchini.
“Kwa kweli tumefikia mahali pazuri, tayari vikao mbalimbali vimefanyika, ikiwamo na viongozi wa Ligi Kuu na FIFA katika kufikia uundwaji wa kamati ya kusimamia Ligi Kuu na Daraja la Kwanza; idadi ya wajumbe na hivyo tuko kwenye hatua za mwisho na Oktoba Kamati ya Utendaji itayaweka hadharani majina hayo,” alisema.
Rais huyo aliongeza kuwa wamefikia uamuzi wa kuunda kamati badala ya kampuni kama ilivyo kwa baadhi ya nchi, ikiwa ni angalizo la kuepukana na migongano kama iliyoko Kenya, Afrika Kusini na Uganda ambapo itapitia kipindi cha mpito cha miaka miwili.
Alifafanua kuwa wajumbe wa kamati hiyo watatoka klabu za Ligi Kuu, Daraja la Kwanza na TFF yenyewe.
Vyanzo: Tanzania Daima na Shaffih
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment