gofu

Chipukizi awapiku wakongwe kuelekea mchezaji bora wa mwaka

MCHEZAJI chipukizi kutoka Klabu ya Gymkhana Arusha (AGC) Nuru Mollel anaongoza kwa pointi katika msimamo wa kuwania kuibuka Mchezaji Gofu Bora Mwaka 2012.

Mollel anaongoza kwa pointi 11 dhidi ya mpinzani wake wa karibu baada ya kukusanya pointi 35 tangu kuanza msimu huu.

Kuongoza kwa Mollel kumechagizwa na mafanikio katika michuano ya karibuni ikiwa ni pamoja na nafasi ya pili aliyoshika kwenye michuano ya Tanzania Amateur Stroke Play iliyomalizika kwenye Viwanja vya Klabu ya TPC Moshi, Kilimanjaro mwishoni mwa wiki iliyopita. Michuano hiyo ya viwanja 54 iliandaliwa na Chama cha Gofu Tanzania.

Chipukizi huyo alikusanya jumla ya mikwaju 209 ikiwa ni mkwaju mmoja zaidi ya bingwa ambaye ni mwenyeji Martin MacDonald aliyekusanya mikwaju 208 katika raundi tatu za michuano hiyo.

Ushindi huo umemfanya MacDonald kushika nafasi ya nne kwenye orodha ya wachezaji wanaoongoza kwa pointi iliyotolewa juzi na TGU akiwa na pointi 18.

Frank Roman wa Moshi anashika nafasi ya pili akiwa na pointi 24, akifuatiwa na Jimmy Mollel wa AGC mwenye pointi 22.

Wachezaji wengine ambao wamejikusanyia pointi kwenye kinyang’anyiro hicho ni Elisante Lembris 14, John Saidi 12 na Isaac Anania 11 wote kutoka AGC na Michael Makala kutoka klabu ya Gymkhana Dar es Salaam mwenye pointi 4.

Katika michuano ya Tanzania Amateur, Roman alishika nafasi ya tatu akiwa na mikwaju 210, wakati Anania alishika nafasi ya nne akiwa na mikwaju 216.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.