MICHUANO ya Taifa ya Gofu ya Wanawake ya Tanzania Open 2012 imepangwa kufanyika kwenye Viwanja vya Klabu ya Gymkhana Arusha baadaye mwaka huu.
Akizungumza na HABARILEO kutoka Morogoro leo, Katibu wa Heshima wa Chama cha Gofu kwa Wanawake Tanzania (TLGU) Anita Siwale alisema michuano hiyo itafanyika Septemba katika tarehe itakayotangazwa baadaye.
Siwale alisema wameamua kupeleka michuano Arusha baada ya Kamati ya Gofu ya Wanawake AGC kuomba kuandaa michuano ya mwaka huu.
“Tulipata ombi kutoka Arusha wakitaka kuandaa michuano ya mwaka huu na tumekubaliana hivyo,” alisema.
Aliongeza kuwa mbali na kuwa wamepata ombi kutoka Arusha chama chake tayari kilikuwa na mpango wa kupeleka michuano ya mwaka huu mkoani humo.
Alisema kuwa Arusha wameahidi kuandaa michuano ya kihistoria mwaka huu.
“Tumefarijika kuona kwamba kuna wanachama wanaoona umuhimu wa kuwa wenyeji wa michuano hiyo, huo ni mfano wa kuigwa,” alisema.
Hata hivyo, michuano hiyo huenda ikawa ndio michuano ya mwisho kwa uongozi ulio madarakani na Rais wa TLGU, Mbonile Burton kwani baada ya hapo kutakuwa na Uchaguzi Mkuu wa viongozi watakaochukua madaraka ya kuongoza kwa kipindi kingine cha miaka miwili ijayo.
Arusha wataandaa michuano hiyo ya taifa kwa mara ya kwanza tangu kufanya hivyo mara ya mwisho mwaka 2008.
0 comments:
Post a Comment