judo

Judo waenda Morocco na matumaini kibao

Cosmas Mlekani

TIMU ya Taifa ya mchezo wa Judo ya Tanzania inatarajia kuondoka nchini kesho kwenda Morocco kushiriki mashindano ya mchujo kusaka tiketi ya kushiriki Michezo ya Olimpiki itakayofanyika baadaye mwaka huu London, Uingereza.

Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi alisema juzi kuwa, ofisi yake imetumia kiasi cha dola za Marekani 12,000 kwa ajili ya kugharimia safari ya wachezaji wanne na kocha mmoja kwenda Morocco.

Alisema mbali na kugharimia nauli, pia TOC itawalipia malazi, chakula pamoja na posho wakati wote timu hiyo itakapokuwa huko, huku usafiri wa ndani wakilipia waandaaji.

Wachezaji watanaotarajia kuondoka kesho ni Andrew Mlungu, Hussein Azzan Khamis, Saniad Abdul Alawi, Juma Mohamed Khamis pamoja na kocha wao Tsuyushi Shimaoka.

Shimaoka akizungumza kwa njia ya simu kutoka Zanzibar jana alisema kuwa, mashindano hayo ni magumu, lakini wana matumaini ya kufanya vizuri na kupata vigezo vya kushiriki Michezo ya Olimpiki itakayofanyika Julai mwaka huu.

“Pamoja na ugumu wa mashindano hayo, lakini tunatarajia kupata matokeo mazuri na kupata vigezo vya kucheza Michezo ya Olimpiki," alisema Shimaoka.

Alisema timu hiyo inatarajia kutua jijini Dar es Salaam leo mchana tayari kwa safari ya Morocco kesho asubuhi.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.