na Mwandishi Wetu
WACHEZAJI kadhaa wamejitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye Uchaguzi Mkuu ujao wa Chama cha Gofu Tanzania (TGU).
Uchaguzi wa TGU ambao ulikuwa ufanyike mapema mwezi huu Klabu ya Gymkhana Arusha umesogezwa mbele hadi Machi 24 kwenye Klabu ya TPC Moshi.
Ofisa Tawala wa TGU, Sophie Nyanjera alithibitisha Dar es Salaam jana majina ya wachezaji waliorudisha fomu za kuwania nafasi za uongozi kwenye Uchaguzi Mkuu ujao.
Katika nafasi ya Mwenyekiti, Paul Matthysen hana mpinzani. Matthysen kwa sasa ni Mwenyekiti wa Muda wa TGU baada ya aliyekuwa Mwenyekiti Dioniz Malinzi kujiuzulu kutokana na kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) mwishoni mwa mwaka jana.
Aliyekuwa Katibu wa Mashindano, Foti Gwebe amejitokeza kuwania nafasi ya Mwenyekiti Msaidizi, wakati Gelase Rutachubirwa ameomba ridhaa ya kuendelea kuwa Mhazini wa TGU.
Julius Mbilinyi amejitosa kuwania nafasi ya Katibu wa Mashindano, wakati nafasi pekee ambayo itakuwa na ushindani mkali ni ya Katibu wa kusimamia viwango vya wachezaji (handicap) ambayo inawaniwa na Akhil Yusufali na Samuel Hagu.
Hata hivyo, Nyanjera alisema hakuna mchezaji aliyejitokeza kuwania nafasi ya Katibu wa Heshima hadi tarehe ya mwisho ya kurudisha fomu ambazo zimepelekwa BMT ambao ndio wasimamizi wa uchaguzi huo.
“Hakuna mtu aliyejitokeza kuwania nafasi ya Katibu wa Heshima, lakini kwa mujibu wa Katiba ya TGU Kamati itakayochaguliwa ina uwezo wa kupendekeza mtu wa kujaza nafasi hiyo,” alisema.
Nafasi hiyo ya Katibu wa Heshima awali ilikuwa ikishikiliwa na Mohamed Sadiki ambaye hajaonesha nia ya kutaka kuendelea.
0 comments:
Post a Comment