WAKATI mwisho wa kurudisha fomu za kugombea nafasi mbalimbali za Uchaguzi Mkuu wa Chama cha Gofu Tanzania (TGU) ni Jumatatu, wagombea wawili tayari wamerudisha fomu hizo.
Uchaguzi Mkuu wa TGU umepangwa kufanyika Machi 24 kwenye Klabu ya TPC Moshi, Kilimanjaro.
Akizungumza na HABARILEO Dar es Salaam jana, Ofisa Tawala wa TGU Sophie Nyanjera alisema baada ya wagombea wote kujaza fomu za awali za chama, walitakiwa kujaza fomu nyingine za serikali ambazo zimetolewa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
“Tayari wagombea wote wamechukua fomu za BMT, lakini hadi sasa ni wawili ambao tayari wamerudisha. Hata hivyo, tunatarajia watarudisha haraka kwani mwisho wa kufanya hiyo ni Jumatatu,” alisema.
Aliwataja wagombea ambao wamerudisha fomu hizo ni Foti Gwebe ambaye anawania nafasi ya Makamu Mwenyekiti na mwanamichezo wa siku nyingi Julius Mbilinyi anayewania ukatibu wa mashindano.
Uchaguzi huo ambao awali ulikuwa ufanyike mapema mwezi huu, Klabu ya Gymkhana Arusha ulisogezwa mbele hadi mwishoni mwa mwezi na kuhamishiwa TPC kwa sababu ambazo hazikuwekwa wazi.
BMT wanatarajia kusimamia uchaguzi huo ambao utatoa viongozi watakaoongoza mchezo huo kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.
0 comments:
Post a Comment