Mbonile Burton
KIKOSI cha wachezaji 8 wa timu ya taifa ya gofu kitakachoshiriki michuano ya Kanda ya Sita Afrika hatimaye kimejulikana.
Akizungumza na HABARILEO kutoka Arusha, jana kocha wa timu ya taifa ya gofu Olais Mollel alisema wachezaji hao wanane wamechujwa kutoka kwenye kikosi cha wachezaji 10 ambao wamepiga kambi Arusha kwa wiki ya pili sasa. Michuano ya Kanda ya Sita Afrika imepangwa kuanza Aprili 16 hadi 19 Lilongwe, Malawi.
Mchezaji huyo wa kulipwa, Mollel aliwataja wachezaji wanaounda kikosi cha timu ya taifa kuwa ni Nuru Mollel, Frank Roman, Jimmy Mollel, Elisante Lembris, John Saidi, Michael Makala, Abas Adam na John Leonce.
Aliwataja wachezaji walioachwa kuwa ni Martin Macdonald na chipukizi Isaac Anania.
Mollel alisema wachezaji hao wanaendelea vema na kambi ambayo ilihamishiwa Arusha badala ya Moshi ambako walitarajia kukaa awali.
Alisema pamoja na hali ngumu ya kifedha wachezaji wanafanya vizuri mazoezini na ana matumaini watafanya vema kwenye michuano ya Malawi.
“Hali ya kifedha sio nzuri sana, lakini wachezaji wanajitahidi kukabiliana nayo, unajua kama baba yako ni masikini huwezi kumkimbia kwa sababu hiyo,” alisema.
Baadhi ya wachezaji pia walikiri ugumu huo, lakini walisema wanatumaini mambo yatakuwa mazuri zaidi watakapoingia kwenye mpambano Malawi.
0 comments:
Post a Comment