gofu

Nahodha wa gofu kushiriki michuano ya A. Kusini

NAHODHA wa timu ya Taifa ya Gofu ya Wanawake Madina Iddi anatarajia kushiriki michuano mikubwa ya wanawake ya Sanlam Afrika Kusini ‘Sanlam Women's Amateur SA Stroke Play Championship’ ambayo itakutanisha wachezaji nyota kutoka nchi mbalimbali za Afrika.

Michuano hiyo ya siku tatu ya viwanja 54 imepangwa kuanza Aprili 15 hadi 17 kwenye viwanja vya Klabu ya Umhlali Country. Michuano hiyo ya kila mwaka yenye upinzani mkali katika Kanda ya Afrika inakutanisha zaidi ya wachezaji 132.

Akizungumza na HABARILEO kutoka Arusha jana Madina alisema anaendelea vema na mazoezi na yupo na ari kubwa ya kuhakikisha anafanya vizuri zaidi mwaka huu baada ya kukosa michuano ya mwaka jana.

“Nimefanya mazoezi ya kutosha, nipo vizuri. Mungu akinisaidia naamini nitapeperusha vema bendera ya Tanzania Afrika Kusini,” alisema Madina anaetarajia kuondoka nchini Aprili 12 kuelekea Afrika Kusini tayari kwa michuano hiyo.

Hiyo, itakuwa mara ya pili kwa Madina kushiriki michuano hiyo ya Sanlam. Mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2010 ambako alifanya vizuri na kufanikiwa kuteuliwa kwenye timu ya kimataifa ambayo ilialikwa kushiriki michuano ya timu baadaye mwaka huo.

Madina pia anatarajia kutumia michuano hiyo kujinoa kwa ajili ya michuano ya Kombe la Challenge Afrika itakayofanyika Gaborone, Botswana Juni.

Kwenye michuano ya Afrika Kusini Madina pia atakutana na wapinzani wake wa karibu kutoka Uganda akiwepo Flavia Namakula, Jaspaer Kamukama na Eva Magala. Mbali na Tanzania na Uganda, wachezaji wengine wanatoka Zimbabwe, Namibia, Botswana na wenyeji Afrika Kusini.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.