gofu

Timu ya taifa ya gofu hadharani wiki hii

Mbonile Burton

KIKOSI cha timu ya taifa ya gofu ya wanaume kitakachoshiriki michuano ya Kanda ya Sita Afrika kinatarajia kujulikana mwishoni mwa wiki hii. Michuano hiyo ya Kanda ya Sita Afrika imepangwa kuanza Aprili 16 hadi 19 Lilongwe, Malawi.

Akizungumza na HABARILEO Dar es Salaam jana, Ofisa Tawala wa Chama cha Gofu Tanzania (TGU) Sophie Nyanjera alisema kati ya wachezaji 10 ambao wameweka kambi Moshi, watachujwa na kubaki 8.

Aliwataja wachezaji ambao wapo kambini kwa zaidi ya wiki ni Nuru Mollel, Frank Roman, Jimmy Mollel, Martin Macdonald, Elisante Lembris, John Saidi, Isaac Anania, Michael Makala, Abas Adam na John Leonce.

Nyanjera alisema timu hiyo imekuwa kambini chini ya kocha mkuu mchezaji wa kulipwa nchini Olais Mollel na Meneja Richard Gomes tangu Machi 26 baada ya kumalizika michuano ya Tanzania Amateur Stroke Play iliyofanyika kwenye viwanja vya Klabu ya TPC Moshi, Kilimanjaro.

“Baada ya kukaa kambini kwa kipindi hicho wachezaji wanatarajia kuchujwa na kubaki nane ambao wataiwakilisha Tanzania kwenye michuano itakayofanyika Malawi,” alisema.

Nyanjera aliongeza kuwa timu hiyo inaendelea vema na mazoezi. Tanzania inajiandaa na michuano hiyo ya kila mwaka ambayo inakutanisha miamba kutoka nchi mbalimbali za Afrika.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.