gofu

Madina Iddi ang’ara Kenya Open

NAHODHA wa timu ya taifa ya gofu ya wanawake ‘The Tanzanite One’, Madina Iddi ametwaa ubingwa wa mashindano ya Wanawake ya Kenya Open.

Mashindano ambayo yalishirikisha wachezaji nyota wa Kenya wakiwepo wa timu ya taifa yamemalizika Mei 6 kwenye viwanja vya Klabu ya Eldoret, Nairobi, Kenya.

Madina aliibuka bingwa baada ya kurejea na mikwaju 78 na kuwashinda wachezaji wengine waliokuwa wakiwania ubingwa. Wachezaji wa Uganda ambao awali pia walitarajia kushiriki hawakutokea.

Akizungumza na
habarileo kutoka Nairobi jana, Madina alisema mashindano yalikuwa mazuri na anashukuru kushinda ingawa alicheza katika wakati mgumu baada ya kupata homa na mafua ghafla.

“Nashukuru kwa kushinda lakini nilitamani kucheza kwa kiwango cha juu zaidi ya nilivyofanya. Wakati wa mazoezi nilikuwa safi, lakini siku moja kabla ya mashindano nilipata homa na mafua makali ambayo yalinifanya siku ya mashindano kuwa na wakati mgumu,” alisema.

Katibu wa Heshima wa Chama cha Gofu kwa Wanawake Tanzania (TLGU), Anita Siwale alisema chama chake kimefurahishwa na maendeleo ya Madina na kujituma kwake.

Mchezaji huyo mwenye kiwango cha uchezaji handicap 3 alitumia mashindano hayo kama moja ya maandalizi ya michuano ya Afrika itakayoanza mapema mwezi ujao Gaborone, Botswana. Michuano hiyo ya Afrika pia itafuatiwa na Botswana Open.

Madina anatarajia kurejea nchini leo baada ya michuano hiyo kabla ya kuanza rasmi kambi ya timu ya taifa.

Hata hivyo, Siwale alisema Madina na Hawa Wanyeche ndio pekee wapo nchini wakati mchezaji mwingine Ayne Magombe aliyekuwa masomoni nje ya nchi anatarajia kuwasili baadaye mwezi huu ili kuanza kambi na wenzake.

“Tumepata taarifa kwamba Ayne tayari amemaliza masomo hivyo, anatumia muda uliopo kujifua na anasubiri kwa hamu kujiunga kwenye timu na wenzake tayari kwa mpambano wa Botswana,” alisema.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.