gofu

Makala aahidi ushirikiano Gofu

Grace Mkojera

NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Amos Makala ameahidi kushirikiana na Timu ya Gofu ya Wanawake katika kushughulikia migogoro na changamoto zinazoikabili timu hiyo ili iweze kufika mbali.

Makala alisema hayo jana wakati akikabidhi bendera kwa timu ya taifa ya Gofu ya wanawake inayotarajiwa kuondoka kesho kwenda kushiriki michuano ya Kombe la Challenge Afrika iliyopangwa kufanyika Gaborone, Botswana kuanzia Juni 5 na 7, na kushiriki pia michuano ya wanawake ya Botswana Open Juni 9 na 10 mwaka huu.

Alisema serikali itaangalia jinsi ya kuwaongezea viwanja ambavyo vitaipa timu hiyo uhuru wa kuutumia kwa shughuli za kimichezo na kwamba vitakuwa huru kwa wanamichezo mbalimbali wanaotaka kufanya mazoezi kushiriki bila matatizo.

“Matatizo yote niachieni mimi kwa vile upele umempata mkunaji, mimi mwenyewe napenda michezo, nitashirikiana na nanyi bega kwa bega ili hatimaye muweze kusonga mbele,” alisema.

Awali, Rais wa Chama cha Gofu Tanzania (TLGU), Mbonile Burton alisema tangu wameingia madarakani mwaka 2010, amekutana na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na migogoro, uhaba wa viwanja na kutopata nyaraka za mawasiliano zinazoonesha utendaji mzima uliokuwa unaendelea siku za nyuma.

Alisema pia, wanapohitaji viwanja vya kufanyia mazoezi hupata shida kwa vile hukutana na vikwazo kwa kuelezwa kuwa sio viwanja vya serikali, hivyo watafute viwanja vyao.

Mbonile alisema wamekuwa wakitumia viwanja vya Gymkhana kufanyia mazoezi lakini wakati mwingine hupewa lugha mbaya na baadhi ya maaskari wa viwanja hivyo, kutokana na hilo hawako huru kwa vile viwanja hivyo vina wanachama wake na sheria zake.

Akikabidhiwa bendera hiyo, nahodha wa timu hiyo Madina Iddi alisema wanaenda kwenye mashindano hayo kwa moyo mmoja wakiamini mwaka huu lazima warudi na kikombe nyumbani, kwa sababu wamejiandaa vya kutosha.

Alisema mwaka 2010 walishika namba mbili kwa sababu hawakuwa vizuri lakini kwa sasa wamejipanga na kujiandaa vizuri hivyo wana matumaini ya kurudi na ubingwa.

Timu hiyo iliyodhaminiwa na Precision Air inaundwa na wachezaji watatu ambao ni Madina Iddi, Hawa Wanyeche na Ayne Magombe, itaongozwa na mkuu wa msafara ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM) na Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mary Chatanda.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.