tenesi

Tango Open kufanyika Juni 23

Grace Mkojera

CHAMA cha Teniis nchini (TTA) kimeandaa michuano ya vijana wa chini ya umri wa miaka 18, itakayojulikana kama Tango Open inayotarajiwa kutimua vumbi Juni 23 na 24 mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Tenisi, Salum Mvita alisema michuano hiyo imedhaminiwa na Tango ambapo itafanyika kwenye viwanja vya Klabu ya Gymkhana na yatashirikisha vijana mbalimbali kutoka mikoa ya Arusha, Mwanza, Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.

Alisema lengo la michuano hiyo ni kuendelea kuunga mkono vipaji vya vijana wenye nia ya kuendeleza mchezo huo ili hatimaye waweze kufikia katika kiwango kizuri cha kuweza kushiriki katika michuano mbalimbali ya kimataifa na hivyo kuitangaza Tanzania kupitia mchezo huo.

“Mashindano hayo yameandaliwa kwa lengo la kuinua vipaji na pia kutumika kuwanoa chipukizi watakaoshiriki michuano ya kimataifa, tunaamini kuwa vijana wengi watajitokeza ili kuonesha vipaji vyao,” alisema.

Alisema kwa sasa maandalizi yanaendelea vizuri na vijana mbalimbali kutoka katika mikoa hiyo wanajiandaa vyema ili kuweza kupambana kwa juhudi na ushindani kwa manufaa yao.

Kwa mujibu wa Mvita, hiyo si michuano ya kwanza kuandaliwa na Tango kwani amekuwa ni mdhamini mkubwa katika michuano mbalimbali ya watoto chini ya umri wa miaka 18, lengo ni kutaka kuhakikisha kuwa mchezo huo unaendelezwa na kupewa heshima kubwa ili vijana wapate moyo wa kuendelea kucheza kwa manufaa yao na nchi.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.