gofu

Tanzania yaalikwa Zambia

TANZANIA imealikwa kushiriki michuano ya gofu ya wazi ya Wanawake Zambia (Zambia Ladies Open) iliyopangwa kufanyika mwezi ujao.

Michuano hiyo ya kila mwaka safari hii imepangwa kuanza Juni 22 hadi 24 kwenye Viwanja vya Klabu ya Nchanga, Chingola.

Akizungumza na HABARILEO kutoka Morogoro jana, Katibu wa Heshima wa Chama cha Gofu kwa Wanawake Tanzania (TLGU) Anita Siwale alithibitisha kupokea mwaliko huo.

“Tumepata mwaliko kutoka kwa Chama cha Gofu kwa Wanawake Zambia (ZLGU) kwa ajili ya kushiriki mashindano yao ya Open,” alisema.

Siwale aliongeza kuwa mwaliko huo uliotumwa na rais wa ZLGU, Moono Mwila unaonesha mashindano hayo ya siku tatu yatakuwa ya viwanja 54.

“Tumepata mwaliko na tayari tumeziandikia klabu mbalimbali kuhusiana na mashindano hayo ili kama kuna wachezaji watapenda kushiriki waanze kujiandaa na kutafuta wadhamini mapema,” alisema.

Siwale alisema mashindano hayo yatafanyika ikiwa ni wiki mbili baada ya michuano ya Afrika itakayofanyika Gaborone, Botswana hivyo, itakuwa wakati mzuri kwa wachezaji nyota nchini kushiriki ili kujipima na wengine.

Aliwataka wachezaji wenye nia ya kushiriki kuanza maandalizi sasa ili kuhakikisha wanafanya vizuri na kuitangaza vema Tanzania.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.