yanga

Maximo kuto kutua yanga

na Dina Ismail

HATIMAYE ‘filamu’ ya ujio wa aliyekuwa Kocha wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, Marcio Maximo kujiunga na Yanga imefikia tamati jana, baada ya uongozi wa klabu hiyo kukiri Mbrazil huyo kutokuja na kuwa wanatarajia kumtangaza kocha mpya wiki ijayo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Mwesiga Selestine alisema, kocha huyo atatoka katika nchi zilizopo Amerika Kusini au Ulaya.

Alisema, uongozi ulipitia maombi ya makocha 25 waliotuma wasifu zao kwa ajili ya kutaka kibarua katika klabu hiyo, ambapo wamewachuja na kubaki watano.

Akizungumzia suala la Maximo, katibu huyo alisema, wameamua kuachana naye kwa vile bado ana mkataba na klabu yake ya Democrata FC ya Rio de Janeiro, Brazil huku pia akipata ofa za kufundisha timu mbalimbali za taifa, ikiwemo Rwanda ‘Amavubi’.

“Kwa sababu hizo, isingekuwa rahisi kumchukua Maximo kufundisha Yanga, kwa mantiki hiyo tumeshafanyia mchujo maombi na kubaki makocha watano, ambapo mmojawapo ndiye atakayekuja kuinoa Yanga,” alisema.

Hivi karibuni, Yanga ilitangaza ujio wa Maximo nchini kwa ajili ya kurithi mikoba ya Mserbia, Kostadin Papic ‘Clinton’ ambaye alitupiwa virago miezi michache kabla ya kumaliza mkataba wake, kutokana na kushindwa kuiletea mafanikio timu hiyo.

Hata hivyo, kadiri siku zilivyokuwa zikisonga mbele, ujio wa Maximo ulibaki kuwa ‘kiza kinene’ huku uongozi ukitoa ahadi kila kukicha, kabla ya jana kukiri kuwa hawezi kuja tena.

Katika hatua nyingine, kikosi cha Yanga kinaendelea na mazoezi yake kwenye Uwanja wa Kaunda chini ya Kocha msaidizi, Fred Felix Minziro, ikiwa ni maandalizi ya michuano ya Kagame inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Julai 14.

About kj

1 comments:

Anonymous said...

Kwa hiyo mzee akilimali anaongea vitu vya uongo na kuwagomba nishawatu kwa kusema vitu asiivyo kuwa na uwakika nacho

Powered by Blogger.