gofu

Tanzania yaanza vizuri gofu Botswana

MICHUANO ya gofu ya Kombe la Challenge Afrika imeanza kwa kasi kwenye viwanja vya Klabu ya Phakalane Resort, Gaborone, Botswana.

Katika raundi ya kwanza juzi timu ya Tanzania ‘Tanzanite Stars’ ilikamata nafasi ya pili ikiwafukuza mabingwa watetezi Afrika Kusini ambao wapo kileleni.

Katika raundi hiyo ya kwanza ya viwanja 18, Tanzania ilikusanya jumla ya mikwaju 153 na kukamata nafasi hiyo wakiwa nyuma ya Afrika Kusini kwa mikwaju 7.

Idadi hiyo ni hatua muhimu kwa Tanzania ambao michuano ya mwisho iliyofanyika Abuja, Nigeria waliachwa kwa zaidi ya mikwaju 13 katika raundi kama hiyo.

Nahodha wa timu ya taifa Madina Iddi aliongoza kwa mfano baada ya kurejea na mikwaju 76 ambayo ni mitatu zaidi ya kiwango cha viwanja hivyo.

Ayne Magombe ambaye alikuwa masomoni Marekani na kurejea nchini wiki iliyopita tayari kuitumikia nchi yake pia alianza vema kwa kupiga mikwaju 77, wakati Hawa Wanyeche hakuwa na siku nzuri aliporejea na mikwaju 82.

Wachezaji wa Tanzania walifanya kazi nzuri na wangeweza kufanya vizuri zaidi kama sio makosa madogo madogo uwanjani.

Hata hivyo, nahodha Madina alisema wapo tayari kupambana hadi dakika ya mwisho na mabingwa Afrika Kusini ambao wamekuwa tishio kwa miaka mingi. Kiwango cha Tanzania pia kimewatisha Afrika Kusini ambao wamesema wataichunga timu hiyo kuhakikisha wanatetea vema taji lao.

Tanzania inashiriki michuano hiyo kwa udhamini wa Precision Air, Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi, Tume ya Mawasiliano ya Taifa (TCRA) na mpenda michezo Asa Mwaipopo.

SOURCE: HABARI LEO

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.