Habari zenu wapenzi wa somaji wa Sports In Bongo, baada ya kupotea katika kipengele cha Wikiend hii 'Pata pa kwenda', imerejea kwa kukujuza sehemu zipi waweza kupata burudani ya michezo nchini Tanzania.
Katika wikend hii kutakuwa na matukio mawili makubwa ambayo ni kuanza kwa michezo ya ligi kuu Tanzania Bara (VPL) na muendelezo wa ligi kuu Zanzibar (ZGPL).
LIGI KUU YA VODACOM (VPL)
Viwanja saba katika mikoa 6 ya Tanzania Bara vitakuwa na kibarua pale wachezaji 22 wakiwa viwanjani kusaka ushindi katika upande wao siku ya jumamosi september 15.
UWANJA WA AZAM, DAR ES SALAAM.
Katika uwanja huo timu zenye upinzani mkali zinazo milikiwa na jeshi la kujenga Taifa (JKT), JKT Ruvu na Ruvu Shooting zitamenyana kusaka point 3 muhimu.
Timu hizo ambazo zilishiriki ligi fupi ya 6 bora za majeshi zilizofanyika katika uwanja wa Mabatini Pwani, na JKT Ruvu kuibuka bingwa.
UWANJA WA TAIFA DAR ES SALAAM.
Simba wawili watakuwa katika uwanja wa Taifa kusaka point 3 muhimu,
Bingwa mtetezi Simba SC watawakaribisha Simba wa Afrika 'African Lyon' ambayo imeweka wazi kuwa wao kipaumbele chao si ubingwa bali ni kuibua wachezaji.
Simba SC ambayo bado haija kaa sawa japo walifanikiwa kuwachalaza Azam FC katika mchezo wa ngao ya Jamii, ushindi ambao unaweza kuwapelekea kufanya vyema katika mchezo huo, ambao, historia inatuonyesha Simba huondokaga na point 3.
African Lyon inayo fundishwa na Mzungu wamekuwa na utamaduni wa kufanya vyema katika mchezo wa kwanza wa ligi kuu.
JAMHURI MOROGORO
Katika mji kasoro bahari timu iliyo rejea ligi kuu Polisi Morogoro watakuwa na kibarua toka kwa jirani zao Mtibwa Sugar.
Polisi Moro ilirejea ligi kuu baada ya kumaliza 9 bora ya ligi daraja la kwanza bila ya kupoteza na mchezo wa mwisho kuwakutanisha na Mtibwa Sugar ilikuwa ni katika michuano ya Super8 bancABC ambapo Polisi Moro walilala kwa Mtibwa Sugar.
SOKOINE MBEYA.
Timu ya jeshi la Magerezo Prisons itakuwa na kibarua cha kuwa timu ya kwanza kuifunga Yanga baada ya kufungwa katika mchezo wa ufunguzi wa kombe la Kagame.
Prisons hawana rikodi nzuri katika uwanja huo, pale wanapo kabiliana na Yanga, ambayo safari hii wanateremka Mbeya wakiwa na safu imara ya ulinzi na ile ya ushambuliaji.
KAITABA, KAGERA
Uwanja wenye rikodi mbaya kwa wageni lakini msimu uliopita katika mzunguko wa kwanza rikodi hiyo iliharibiwa baada ya timu waalikwa kuambulia point katika uwanja huo unao tumiwa na Kagera Sugar.
Azam ambao hawajawahi kuondoka na point 3 zote katika uwanja huo watakuwa na kibaruwa cha kufanya hivyo kwa mara ya kwanza watakapo wakabili wenyeji wao Kagera Sugar.
CCM KIRUMBA, MWANZA
Toto African ndio timu inayotazamiwa kuwa na wakati mgumu msimu huu, na kuonekana kuwa ni miongoni mwa timu zinazopewa nafasi kubwa ya kushuka daraja, watakuwa na kibarua toka kwa tumaini jipya la Arusha JKT Oljoro.
Toto Africa wamekuwa na utamaduni wa kufanya vyema katika michezo ya mwanzo, na kasi yao kupungua kadri ligi inapozidi kusogea mbele.
MKWAKWANI, TANGA
Wakazi wa Tanga watakuwa katika uwanja wa Mkwakwani kushuhudi wawakilishi wao wakimenyana na kusaka point 3 muhimu.
Coastal Union inayopewa nafasi ya kufanya vyema msimu huu, japo wamekuwa na matokeo mabovu katika michezo ya kirafika watakuwa wageni wa mgeni wa VPL Mgambo JKT.
LIGI KUU YA ZANZIBAR GRAND MALT (ZGPL).
Ligi kuu ya Zanzibar Grand Malt wikiend hii inaingia katika raundi ya pili ambapo kutakuwa na michezo minne ambapo miwili itachezwa jumamosi na mingine jumapili.
JUMAMOSI SEPTEMBER 15.
SUPER FALCON Vs DUMA
Mabingwa watetezi Super Falcon walio anza vibaya ligi hiyo kwa kuchapwa goli 2-0, watakuwa wanajaribu bahati yao katika uwanja wa Gombani kisiwani Pemba mbele ya Duma waliopoteza mchezo wao wa kwanza toka kwa Jamhuri.
KMKM Vs MALINDI
Katika uwanja wa Amaan uliopo unguja Mabaharia wa KMKM ambao walipoteza 1-0 kutoka kwa Mafunzo, watakabiliana na Malindi ambao nao katika mechi yao ya kwanza walipoteza dhidi ya Bandari 3-2.
JUMAPILI SEPTEMBER 16
MAFUNZO Vs BANDARI, U/Amaan CHIPUKIZI Vs JAMHURI, Gombani
0 comments:
Post a Comment