vilabu

PRISONS YATOLEWA NISHAI KYELA

TIMU ya Tanzania Prisons ya jijini Mbeya inayoshiriki Ligi Kuu Bara
imeadhiriwa na watoto wa mchangani katika mchezo wa kirafiki
uliofanyika Uwanja wa John Mwakangale (Shamba la Babu), uliopo
kitongoji cha Bondeni, Kata ya Kyela mjini hapa baada ya kukubali
kichapo cha bao 1-0, juzi.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Katibu Mkuu wa Chama cha Soka
Wilaya ya Kyela (KDFA), Evans Mwandemani alisema kuwa waliomba kucheza
mchezo wa kujipima nguvu na timu hiyo na wao wakaamua kukusanya vijana
walio chini ya miaka 20 kutoka kata mbalimbali na kuunda kombaini
ambayo ilifanikiwa kutoa kichapo kwa maafande huo.

Alisema kuwa aliamua kuwaacha wachezaji wenye majina na kuwatumia
vijana wasiokuwa na majina, ambao walikaa kambini siku mbili huku
wakiwa wanapata maelekezo ya kujiamini uwanjani chini ya kocha Godfrey
Katepa, ambayo yalizaa matunda baada ya ushindi wa bao hilo
lililopatikana dakika ya 70, mfungaji akiwa Askofu Kipene 'Fabregas'.

Naye Mwenyekiti wa KDFA, James Mwakilema alisema timu hiyo ilionyesha
uwezo wa hali ya juu uwanjani na kwamba, kilichosababisha ni jinsi
walivyopata maelekezo ya kuwajenga kisaikolojia na kwa hali hiyo, wao
kama chama wataifanya timu hiyo kuwa ya wilaya ili iweze kufanya
vizuri zaidi kama Kyela Stars.

Mwakilema alimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Magret Marenga kwa
kuwawezesha vijana hao tangu walivyokuwa kambini na kumsihi asisite
kuisaidia timu hiyo katika michezo mingine, kwani katika mchezo huo
uliohudhuriwa na viongozi wa halmashuri akiwemo Kaimu Mkurugenzi
Joseph Njau, Ofisa Utamaduni, Kasmini Mfaume, DC mwenyewe na viongozi
wengine waandamizi, wachezaji walionyesha thamani yao kwa kuichapa
timu hiyo kama asante kwa mkuu huyo wa wilaya kwa mchango wake.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, David Mwamwaja
alipohojiwa kuhusiana na matokeo hayo, alisema ni sawa timu yake
imefungwa, lakini kumetokana na wachezaji wake sita tegemeo kuwa
majeruhi, na kwamba atakuja tena kucheza na timu hiyo kwani
wameonyesha soka safi na ya kuvutia.

Kuhusu mpango mkakati walionao katika kujinasua kutoka nafasi
waliyonayo katika Ligi Kuu Bara na kusogea nafasi za juu, Mwamwaja
alisema tayari wamekwishajiandaa vya kutosha na watafanya vizuri
katika mechi zao za mzunguko wa pili na suala la kushuka daraja kwao
ni ndoto, wataushangaza umma.


CHANZO: TANZANIA DAIMA

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.